Halmashauri ya wilaya ya Ileje mkoani Songwe, imeadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuainisha mafanikio makubwa ya kimaendeleo na kuitaka jamii kuendelea kushirikiana kuwalinda watoto na kukemea matukio ya ukatili na unyanyasaji hasa kwa watoto.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika kata ya Itale wilayani Ileje yakihudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali na wanafunzi wa shule mbalimbali wilayani humo.
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mheshimiwa Farida Mgomi, ambaye ametumia maadhimisho hayo kuwahimiza wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawalinda watoto na kuwa mstari wa mbele kutetea haki za watoto, ikiwa ni ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao kwa kuwa daraja la mafanikio yao ya baadaye.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa DC Mgomi ametoa rai kwa jamii kuepuka na kukemea vikali vitendo na viashiria vyote vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, akisisitiza kuwa kila mtoto anapaswa kulelewa katika mazingira salama na yenye heshima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwapatia watoto mahitaji ya msingi kama vile lishe bora, huduma za afya, elimu na malezi yenye upendo ili kuwawezesha kukua katika hali bora kimwili na kiakili na kuzitaka familia kuhakikisha zinawashirikisha watoto katika maamuzi yanayowahusu na kuhakikisha ulinzi na usalama wao (watoto).
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Ileje bi. Farida Salum Mgomi, ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mmoja katika jamii hivyo wadau wote hawana budi kushirikiana katika kuhakikisha watoto wa wilaya ya Ileje na Tanzania kwa ujumla wanalelewa katika misingi ya haki, usawa na utu ili kuwasaidia katika makuzi yao na kufikia ndoto zao.
0 Comments