Na Josea Sinkala, Mbeya.
Jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilayani Mbeya imeeleza kujipanga na uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa maelezo kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo umekuwa mzuri na wenye kuridhisha.
Kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo wilayani Mbeya, Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake wamekuwa wakieleza kutembea kifua mbele na kwamba kwa utekelezaji huo wa miradi ni wazi kwamba CCM itashinda kwa kishindo uchaguzi huo wa mwaka huu.
Gabriel Kilembe afisa kutoka ofisi ya Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza na pia ndiye Katibu wa jumuiya ya vijana kata ya Isangala (kichama), amesema Serikali hasa ya awamu ya sita imefanya mambo mengi ikiwemo ujenzi wa barabara, uboreshaji miundombinu ya elimu, huduma za afya na mambo mengine mbalimbali.
Kilembe amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Iwindi na kata ya kichama Isangala hususani vijana waliokuwa kwenye bonanza la michezo (mpira wa miguu) ambalo pia limeungwa mkono kwa asilimia kubwa na Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza ili kuendelea kuwaunganisha vijana na wana michezo kwa ujumla.
Pamoja na hayo amesema ofisi ya Mbunge inaendelea kuikumbusha Serikali juu ya maswala mbalimbali ya kuyatatua katika jamii kama ambavyo kero mbalimbali zimeendelea kutatuliwa na kuwaasa vijana kuwa kipaumbele kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Iwindi Mhe. Admin Mfisile Nswila, amesema kata yake ilikuwa nyuma kimaendeleo lakini sasa miradi mbalimbali imejengwa kwa kiwango cha juu na Serikali kwa ushawishi na ushirikiano wake na Mhe. Mbunge wa Mbeya vijijini.Ametaja baadhi ya miradi kuwa ni umeme ambao umefika kwenye vijiji vyote na sasa unasambazwa vitongojini, ujenzi wa barabara kadhaa na madaraja, ujenzi vyumba vya madarasa zaidi ya 25, upatikanaji wa shule pekee ya wavulana katani humo, ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Mbeya na miradi mingine lukuki hivyo kuipigia debe CCM kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
0 Comments