Uamuzi wa Rais wa Marekani,Donald Trump, kusitisha shughuli za shirika la Maendeleo ya kimataifa la Marekani(USAID) kumesababisha kusimama miradi yenye thamani ya zaidi ya trilioni moja na kufungwa kwa ofisi kadhaa za asasi za kiraia huku mamia ya wafanyakazi wakikosa ajira.
Rais Trump mwezi Februari mwaka huu, alitangaza kusitisha asilimia 80 ya miradi ambayo imekuwa ikifadhiliwa na USAID katika nchi kadhaa duniani, kwa kile ambacho alieleza kupunguza matumizi ya serikali yake .
Akiwasilisha taarifa ya utafiti uliofanywa na Mtandao wa mashirika ya watetezi wa haki za binaadamu nchini(THRDC),kuhusiana na athari za USAID kujiondoa ghafla na uhimilivu wa asasi za kiraia nchini,katika maadhimisho ya wiki ya azaki 2025 jijini Arusha, Mratibu wa kitaifa wa THRDC Wakili Onesmo ole Ngurumwa alisema imebainika asilimia 50 ya Azaki nchini zilizokuwa zinapata fedha kutoka USAID zimeathirika sana.
Ole Ngurumwa alisema katika utafiti huo ambao bado takwimu zinakusanywa, uliotokana na dodoso lililojazwa na azaki nchini,imebainika kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa ni mashirika makubwa ya kimataifa , mashirika ya dini,mashirika yaliyokuwa na miradi ya afya, uhifadhi na mazingira ,miradi ya maji, masuala ya haki za binaadamu na masuala ya ukuzaji demokrasi na utawala bora nchini.
" Kuna mashirika yamefunga ofisi, mengine yamepunguza wafanyakazi, mengine yanakabiliwa na ukata mkubwa na mwaka huu tuna uchaguzi mkuu USAID kupitia mashirika yake makubwa wamekuwa wakitoa ufadhili wa Azaki ili zitowe elimu ya mpiga kura na nyingine kuwa waangalizi wa uchaguzi mwaka huu fedha zao hakuna hivyo ushiriki za azaki katika uchaguzi utapungua sana "alisema
Alisema katika utafiti huo. imebainika kuwa mchango wa sekta ya Azaki nchini kwa taifa unatarajiwa kupungua kwa zaidi ya asimilia 50, ambapo takwimu zinaonesha mwaka uliopita mchango ulifikia zaidi ya trilioni mbili ambapo USAID ndio walikuwa wafadhili wakubwa wa miradi nchini.
" Kwa takwimu tulizonazo Kwa mwaka 2023 Tanzania ilipokea Dola milioni 630 (takriban Sh. Trilioni 1.61) na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi 20 zilizoongoza kwa kupokea misaada kutoka USAID huku ikishika nafasi ya 10 duniani na ya 10 barani Afrika na tunatarajia kukutana na Ubalozi wa Marekani hapa nchini kupata takwimu zaidi"alisema.
Alisema kilichotokea kutokana na USAID kusitisha ufadhili ni fundisho kubwa kwa Azaki na sasa zinapaswa kuanza kutafakari na kuwa na mikakati mipya ya kuwa na uhimilivu katika mapato na kutafuta mbinu mpya za kujipatia ufadhili wa miradi badala ya kutegemea kutoka nje ya nchi pekee.
" Tunaendelea na majadiliano katika maadhimisho haya kuona jinsi gani Azaki zinaweza kuhimili hali ya sasa ya kupungua kwa ufadhili kutoka mashirika makubwa ya kimataifa na kujengeana uwezo wa mbinu mbadala"alisema
0 Comments