Header Ads Widget

SHEIKH KIVUMA WANAOCHAFUA AMANI WANA NAULI KUKIMBILIA SISI HATUNA


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

MKURUGENZI wa Madrasa na Daawa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Yahaya Kivuma, amewataka Watanzania kutoruhusu kuchochewa kuvuruga amani ya taifa, akisisitiza kuwa mara nyingi wanaoanzisha vurugu huwa na uwezo wa kukimbilia mataifa mengine, tofauti na wananchi wa kawaida.

Akihutubia waumini wa Kiislamu kwenye Swala ya Eid El-Adha iliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Sheikh Kivuma alisema ni jukumu la kila Mtanzania kulinda amani iliyopo kwa gharama yoyote ile. 

"Ndugu zangu Waislamu, asitokee mtu yeyote akawalisha sumu ya kuchafua amani. Wanaochafua amani mara nyingi huwa na nauli ya kukimbia, lakini sisi wananchi wa kawaida hatuna. Tuihifadhi amani hii kwa nguvu zetu zote,” alisema.

Sheikh Kivuma aliongeza kuwa mataifa mengi yameathirika kwa migogoro ya ndani, na kwamba Tanzania imekuwa kimbilio kwa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa sababu ya utulivu wake. Alisisitiza kuwa amani ni msingi wa afya ya taifa, na bila amani, hakuna shughuli yoyote inayoweza kufanyika.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Swed Twaibu, aliwataka Watanzania kuendelea kuiombea nchi, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Tunapaswa kuwa na subira hadi pale viongozi wapya watakapotangazwa. Tuache maneno au matendo yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi yetu,” alieleza.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Mustafa Rajab, aliwahimiza waumini wa Kiislamu wenye sifa na uwezo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwa ni pamoja na ubunge na udiwani, akiwataka kuwa viongozi wa haki iwapo watapata nafasi hiyo.

“Ni muhimu kila Mtanzania mwenye sifa kuchukua hatua na kugombea nafasi. Lakini tukumbuke kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo. Bila amani, hakuna litakalofanyika,” alisema.

Sheikh Mustafa pia alikumbusha umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye ibada ya kuchinja kwa ajili ya Eid El-Adha, kwa kuwashirikisha watu wenye uhitaji.

“Wenye uwezo wa kuchinja wanapaswa kuwajali wasiokuwa na uwezo kwa kuwagawia kitoweo. Ni aibu mtu mwenye uwezo kugombania nyama, wakati wengine hawana hata kipande,” alisisitiza.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI