Na Matukio Daima Media, Iringa
Baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Kilolo, mkoani Iringa, wametoa wito kwa mdau wa maendeleo na kada wa muda mrefu wa chama hicho, Aidan Mlawa, kutangaza mapema nia yake ya kuwania ubunge wa jimbo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Matukio Daima, wanachama hao wamesema Mlawa amekuwa akionesha moyo wa kujitoa kusaidia maendeleo ya wananchi wa Kilolo na hata nje ya mipaka ya wilaya hiyo, hali inayowapa matumaini kuwa atakuwa kiongozi bora iwapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia kupitia nafasi ya ubunge.
Adiliano Kikoti, mkazi wa Kidabaga na mwanachama wa CCM, alisema Mlawa ni mmoja wa makada wanaohitajika kwa sasa ndani ya chama kutokana na mchango wake mkubwa katika kuunga mkono shughuli za kijamii, elimu, afya, michezo na maendeleo ya vijana.
“Kuna umuhimu mkubwa kwa ndugu Mlawa kutangaza nia mapema. Hii itatufanya sisi wana CCM kumuunga mkono kwa maandalizi ya kutosha na pia kutufanya tuanze kujipanga kisaikolojia kwa mabadiliko tunayoyataka ameonyesha kuwa ni mzalendo wa kweli na ana maono makubwa kwa Kilolo,” alisema Kikoti.
Naye Amina Ally, mwanachama kutoka Kata ya Ilula, alisema Mlawa ameendelea kuwa msaada mkubwa kwa jamii, si tu kwa kutoa misaada ya vifaa vya shule na afya, bali pia kwa kuhamasisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM.
“Tumeona matendo yake kwa muda mrefu. Hafanyi kwa ajili ya kampeni bali ni utaratibu wake wa kawaida kusaidia watu. Tunaamini sasa ni wakati wake wa kuingia katika ulingo wa kisiasa rasmi kwa kuwa mwakilishi wetu bungeni,” alisema Amina.
Wanachama hao wamesema pamoja na heshima waliyonayo kwa viongozi waliopo, wanaamini ni muda sahihi wa kuibua damu mpya yenye fikra mbadala na shauku ya kweli ya kuwatumikia wananchi wa Kilolo kwa moyo wa kizalendo na ufanisi zaidi.
Wamesema wanatamani kuona Mlawa akitangaza rasmi nia yake ndani ya miezi michache ijayo, ili wapate fursa ya kuanza harakati za kuhakikisha anashinda mchujo wa ndani ya chama na hatimaye kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa 2025.
Kwa upande wake, Mlawa alipoulizwa kuhusu wito huo wa wanachama, alisema anashukuru kwa heshima hiyo na anaendelea kutafakari kwa kina pamoja na kushauriana na familia, wazee wa chama na viongozi wa maeneo mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
“Nawashukuru sana kwa heshima hii kubwa. Mimi ni mwana CCM wa kweli na nitakuwa tayari kutumikia chama na wananchi katika nafasi yoyote nitakayopaswa kuwepo, lakini kwa sasa naendelea kusikiliza maoni na ushauri,” alisema Mlawa.
Hadi sasa Mlawa mwenyewe bado hajasema chochote kama atagombea ubunge jimbo la Kilolo ama lah na ukimya wake ndio umesukuma wana CCM hao kumshawishi kutangaza nia.
Jimbo la Kilolo ni miongoni mwa majimbo ya mkoa wa Iringa yanayotarajiwa kushuhudia ushindani mkali wa kisiasa kuelekea uchaguzi ujao, huku hamasa ya vijana na makada wapya wa CCM ikizidi kushika kasi.
0 Comments