Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imezindua zoezi la kulinda mazalia na makulia ya samaki katika Ziwa Victoria kwa kuweka maboya 32 kwenye mipaka ya maeneo maalumu yaliyotengwa ambayo hayataruhusiwa kuvua samaki.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, alizindua zoezi hilo katika eneo la mwalo wa Shadi ndani ya Ziwa Victoria na kusema serikali inafanya hivyo ili kudhibiti uvuvi haramu kwenye maeneo maalumu yaliotengwa katika ziwa hilo.
Alisema suala la kuweka alama katika maeneo mahususi yaliobainishwa kwa ajili ya mazalia na makulia ya samaki ni takwa la kikanuni na maeneo haya yamebainishwa kwa kushirikiana na Mmmaafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau wa sekta ya uvuvi.
“Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji amenituma kuja kuweka alama za maboya kwenye maeneo yalioainishwa kama mazalia ya Samaki na vilevile kuja kupandikiza vifaranga vya samaki 10,000 katika mwalo wa Shadi, hapa Ziwa Victoria, japo tayari tulishapandikiza vifaranga 1,231,000 katika Ziwa Ikimba mkoani Kagera,” aliseama Dk. Mhede.
Dk. Mhede alisema hategemei kuona wavuvi wakiharibu au kuvua samaki katika maeneo haya yaliyobainishwa kwa ajili ya mazalia na makulia ya samaki na kuvitaka Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kusimamia na kutoa taarifa wanapoona kuna wavuvi wanaokiuka utaratibu uliowekwa.
Alisema sekta ya uvuvi inatoa fursa ya uvuvi kwa mwananchi na kuna takribani mahitaji ya samaki tani laki saba kwa mwaka ambayo inahitaji wadau wajitokeze katika kuwekeza na kuzalisha ili kuweza kufikia lengo na hivyo kuongeza pato la mtu moja na pato la taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa Serikali ina mpango kabambe wa miaka kumi ulioanzishwa 2022 na utaenda mpaka hadi 2037 kuhakikisha sekta ya uvuvi inachochea mapinduzi ya uchumi wa buluu nchini.
Naye Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh alisema mkakati wa kulinda mazalia ya samaki ni mkubwa kwa sababu katika maeneo ya ziwa na bahari kuna changamoto nyingi ikiwemo mambo ya athari za tabia ya nchi na ongezeko la watu linalosababisha mahitaji ya samaki kuongezeka na samaki kupungua.
Alisema yapo maeneo zaidi ya 100 ambayo ni mazalia ya samaki ambayo yanahitaji kuwekewa maboya na uwekaji huo umekuwa shirikishi kwa kuwashirikisha wadau wa uvuvi na wamekubali kulinda maeneo haya ya mazalia.
Prof. Sheikh alisema maboya haya yana ubora mkubwa na yana uwezo wa kuishi kwa miaka 80 kama yakitunzwa vizuri na yametengenezwa na Chuo kikuu cha Dar es Salaam ili kusaidia katika uzalishaji wa samaki katika Ziwa Victoria.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Mkilagi alimshukru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuleta maboya katika Ziwa Victoria ambayo yatasaidia katika uzalishaji wa samaki na kukuza shughuli za uchumi Mwanza na kupungua shughuli za uvuvi haramu nchini.
MWISHO
0 Comments