Header Ads Widget

WAZIRI BASHE ATOA TAARIFA YA MAFANIKIO YA SEKTA YA KILIMO BUNGENI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima  App Dodoma

WAZIRI wa Kilimo,Hussein Bashe, leo Mei 21, 2025, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, akieleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika hotuba yake, Waziri Bashe alieleza kuwa Wizara ya Kilimo imenunua jumla ya matrekta makubwa 500 na matrekta madogo 800 (power tillers) kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakulima kote nchini. Vifaa hivyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza tija kwenye kilimo.

Aidha, serikali imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kusindika zabibu chenye uwezo wa kuchakata tani 300 kwa mwaka katika Mkoa wa Dodoma, pamoja na Kituo Mahiri cha Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna kilichopo Mtanana, mkoani humo.

Ajira Milioni 1.08 Zimezalishwa

Akizungumzia mchango wa sekta ya kilimo katika ajira, Waziri Bashe alisema kuwa serikali kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo imeweza kuzalisha ajira 1,084,481 ikiwa ni pamoja na za muda mfupi na za kudumu. Ajira hizo zinatokana na miradi ya utafiti, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora, na Vyama vya Ushirika.

Usambazaji wa Pembejeo kwa Mazao ya Kimkakati

Waziri Bashe alisema kuwa katika zao la korosho, serikali imewezesha upatikanaji na usambazaji wa salfa ya unga tani 109,083.695, viuatilifu vya maji lita 8,823,687.5 pamoja na mabomba ya kunyunyizia viuatilifu 6,337, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi 556,719,057,804.95 kupitia mpango wa ruzuku.

Kwa upande wa tumbaku, serikali imesambaza pembejeo zikiwemo mbolea, viuatilifu na vifungashio vyenye thamani ya Shilingi 607,292,419,460.43.

Kwa zao la pamba, serikali imewezesha upatikanaji wa mbegu, mbolea na viuatilifu vyenye thamani ya Shilingi 325,361,502,000.

Miradi ya Umwagiliaji Yafikia 780

Waziri Bashe alisema miradi ya umwagiliaji imeongezeka kutoka miradi 13 mwaka 2020/2021 hadi 780 mwaka 2024/2025, ikihusisha eneo la zaidi ya hekta 543,366. Kukamilika kwa miradi hii kunatarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji hadi kufikia hekta 1,270,647.

Aidha, idadi ya Vyama vya Umwagiliaji vilivyosajiliwa imeongezeka kutoka 19 hadi 912. Serikali pia imefungua ofisi 121 za wilaya, kuajiri watumishi 344, na kununua mitambo 30, magari makubwa 17, mitambo 18 ya kuchimba visima, pamoja na magari madogo 58 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hiyo.

Mageuzi Katika Vyama vya Ushirika

Waziri huyo pia alibainisha hatua zilizochukuliwa kuimarisha vyama vya ushirika, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika Tanzania yenye mtaji wa Shilingi Bilioni 58 na matawi katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Mtwara na Kilimanjaro.

Mafanikio mengine yaliyotajwa ni pamoja na usambazaji wa mizani ya kidijiti 3,760 kwa vyama 992, ongezeko la ajira katika vyama vya ushirika kutoka 100,100 hadi 155,106, pamoja na kuongezeka kwa viwanda vya ushirika hadi kufikia 331.

Akiba za wanachama katika SACCOS zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 576 hadi Bilioni 966.9, huku mikopo ikipanda kutoka Shilingi Bilioni 798 hadi Trilioni 1.1.

Idadi ya vyama vilivyopata hati safi imeongezeka kutoka 339 hadi 631, wakati vyenye hati chafu vimepungua kutoka 2,075 hadi 995.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI