Na Shomari Binda-Musoma
WAKANDARASI wawili wameendelea na kasi ya kazi ya usambazaji wa umeme kwenye vitongoji baada ya kukamilisha kwenye vijiji kwa asilimia 100.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya mbunge wa jimbo hilo jana mei 10,2025 imesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 sasa kazi inaendelea kwenye vitongoji 74 ambayo inatarajiwa kukamilishwa disemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo imesema vitakapokamilika Vitongoji hivyo jimbo hilo litakuwa limebakiza Vitongoji 100 kati ya 374 na kufikia asilimia 73.26.
Kwa mwaka wa Fedha 2025/26 Vitongoji 50 kati ya 100 vilivosalia kazi ya usambazaji itaanza 1.7.2025 ili kufikishiwa umeme.
Vijiji 68 kwenye Kata 21 vilivyopo kwenye jimbo hilo tayari vimefikiwa na huduma ya umeme ikiwa ni sawa na asilimia 100.
Kwa upande wa wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Jimbo la Musoma Vijijini wanatoa shukrani nyingi kwa serikali inayoongozwa vizuri na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo na ustawi wa Jimbo hilo
Magesa Juma mkazi wa Kijiji cha Butata Kata ya Bukima amesema umeme umewasaidia sana kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kiuchumi.
Amesema umeme umesaidia vijana kuanzisha salon za kunyoa ambazo zimewasaidia kupata kipato ambacho kimeweza kuwasaidia
" Tunaishukuru serikali kwa miradi ya umeme ambayo imekuja kutusaidia kwenye vijiji vyetu na sasa unazidi kusambaa kwenye Vitongoji vyetu.
"Tunamshukuru sana pia mbunge wetu Profesa Sospeter Muhongo amekuwa msaada wetu kwa ufatiliaji wake kuhakikisha miradi mbalimbali inatufikia",amesema.
0 Comments