Na Matukio Daima App, Itilima.
FISI wanne ameingia katika Kijiji cha Gambasingu wilayani Itilima Mkoani Simiyu, na kuvamia zizi la kondoo kisha kuua kondoo 17 huku wengine watano wakijeruhiwa katika shambulio la usiku wa kuamkia Agosti 21,2025.
Tukio hilo kusikitisha ambalo limeacha simanzi na umaskini, lilitokea majira ya saa sita usiku katika Kitongoji cha Mwabasambo A, ambapo limeelezwa na wenyeji kuwa ni tukio la kihistoria kutokana na idadi kubwa ya mifugo kushambuliwa kwa wakati mmoja.
Singisi Mgina, mfugaji aliyeathirika akizungumza jana kijijini hapo amesema fisi hao walivamia zizi lake kwa kasi na kuua kondoo kabla hajapata msaada wa kupiga yowe.
“Walivamia ghafla na kuua kondoo kwa muda mfupi. Nilipopiga kelele wananchi walifika lakini tulishindwa kuwafukuza...Hasara yangu ni kubwa, inafikia Shilingi Mil. mbili, Kondoo hawa ndio chanzo cha kipato cha familia yangu,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Gambasingu, Buka Maduhu, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa idadi kubwa ya kondoo waliouawa inaashiria ukali wa tatizo.
Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Itilima, Nelson Kira, amesema serikali imeanza msako kwa kushirikiana na wananchi na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Mwisho.
0 Comments