Header Ads Widget

VIONGOZI WA DINI, SIASA, SERIKALI NA MILA MKOANI SONGWE WATOA WITO WA KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO.


Na Moses Ng'wat, Mbozi.

Katika jitihada za kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kulinda misingi ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Songwe limeongoza dua maalum ya kuombea amani ya nchi.

Tukio hilo limefanyika leo, Mei 17, 2025, katika shule ya sekondari Vwawa, wilayani Mbozi, na kuwahusisha viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa, serikali pamoja na viongozi wa kimila, lengo likiwa kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na taifa kwa ujumla, kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Viongozi wote waliohudhuria waliungana kwa sauti moja kulaani matamshi, mienendo na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi, wakisisitiza kuwa amani ni rasilimali adimu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya chama chake, Katibu wa UDP Mkoa wa Songwe, Daud Myombe, alitangaza rasmi kuwa chama hicho kitaunga mkono mgombea wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kinyang’anyiro cha urais. 

Alisema hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazoendelea nchini, na kuwataka wananchi wa Songwe kuwachagua wagombea wa UDP katika nafasi za ubunge na udiwani.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAUMA mkoani humo, Nikubuka Kayuni, alipongeza mazingira ya kisiasa kuwa huru na ya haki, akisema hali hiyo imewawezesha wanasiasa na vyama vyao kufanya shughuli bila bugudha.

Mgeni rasmi katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alisisitiza kuwa jukumu la kudumisha amani ni la kila mmoja – kuanzia kwa raia wa kawaida hadi kwa viongozi wa dini, siasa na serikali.

“Ninatoa rai kwa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao kushiriki kwenye uchaguzi kwa njia ya kistaarabu – bila matusi, vitisho wala uchochezi. Amani ni msingi wa maendeleo, tusikubali kuitumbukiza nchi kwenye machafuko,” alisisitiza Mwandobo.

Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetumia zaidi ya shilingi bilioni 758 katika Mkoa wa Songwe kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo elimu, afya, barabara, maji, umeme, kilimo na uwekezaji. Alisema kiasi hicho ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya serikali kuuinua mkoa huo kiuchumi na kijamii.

“Kwa niaba ya Serikali ya Mkoa na kwa nafasi yangu, napenda kutoa shukrani kwa uongozi wa BAKWATA na wadau wote walioandaa dua hii ya kitaifa. Hii ni ishara ya uzalendo, mshikamano na imani yetu kwa Mungu na taifa letu,” aliongeza.

Awali, akiwasilisha ujumbe wake, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Hussein Batuza, alisema dua hiyo imelenga kuiombea nchi haki, utulivu na uchaguzi wa amani. Alitoa onyo kwa watu au viongozi wenye nia ya kuvuruga amani kwa misingi ya kidini au kisiasa.

“Watanzania tuilinde amani yetu. Tuwakatae wanaotaka kutugawa kwa misingi ya udini au vyama. Viongozi wa dini mnayo nafasi ya kuishauri serikali kwa hekima, siyo kuiamrisha,” alisema kwa msisitizo.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI