Na Shomari Binda-Musoma
Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini( TARURA) na Wakala wa Barabara Nchini( TANROADS) mkoa wa Mara wameahidi kutoa kazi kwa vikundi vitakavyosajiliwa kwaajili ya kutunza na kuhudumia barabara.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TARURA mkoa wa Mara Mhandisi William Lameck alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 14 kwa wanawake,vijana na makundi maalum watakao hudumia barabara.
Amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa mkoa wa Mara katika kuhakikisha wanashirikiana kutunza na kulinda barabara.
Mhandisi William amesema watu 86 waliopata mafunzo hayo wanapaswa kuchangamkia fursa na kuanzisha vikundi kwa haraka ili waweze kupata kazi na kujipatia kipato na kujiinua kiuchumi.
" Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka na kazi zipo na tupo tayari kuwapa kazi kupitia vikundi mtakavyovianzisha ili muweze kuzihudumia barabara zetu.
" Nimpongeze na kumshukuru mhandisi Magesa Mwita kwa kuliona hili na kuamua kuleta mafunzo haya kwa kuyawezesha kwa wananchi wa mkoa wa Mara",amesema.
Mkufunzi wa mafunzo hayo mhandisi Frenk Kisandi kutoka taasisi ya teknolojia ya ujenzi mkoani Mbeya amesema dhamira ya mafunzo ni kupata uelewa na kwenda kuzihudumia barabara pasipo kutumia vifaa vya gharama kubwa.
Amesema mafunzo waliyowapa wahitimu hao 86 ambao wanaweza kuanzisha vikundi vya watu zaidi ya 400 ni ya nadhalia na vitendo na taratibu za utunzaji wa barabara,madaraja na kalavati.
Kwa upande wa mwezeshaji wa mafunzo hayo nhandisi Mwita Magesa kutoka Tanroads mkoa wa Mwanza amesema kama mzaliwa wa mkoa wa Mara nakuona hakuna vikyndi vya kutosha kufanya kazi hizo ameamua kusaidia kuleta mafunzo hayo.
Amesema anaamini fursa hiyo ikitumiwa kwa lengo lililokudsudiwa itasaidia vikundi vitakavyoanzishwa na waliopata mafunzo kufanya kazi za kutunza barabara kwa kuzihudumia na kujiwezesha kiuchumi.
Moja ya wanufaika wa mafunzo hayo Emanuel Bwimbo wamemshukuru mhandisi Mwita Magesa kwa kuwaletea mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuanzisha vikundi hivyo tayari kwa kuanza kazi.
0 Comments