Header Ads Widget

UPOTEVU MAJI SAFI WASABABISHA HASARA YA BILIONI 2 KUWASA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  Kigoma Ujiji (KUWASA) inapoteza kiasi cha Shilingi Bilion mbili  kila mwaka kutokana na upotevu wa maji ambapo  asilimia 41 ya maji safi yaliyotiwa dawa  yanayopotea kutokana na uchakavu wa miundo mbinu.

Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Poas Kilangi alisema hayo akitoa taarifa wakati wa uzinduzi wa mfumo  wa utoaji taarifa za mivujo ya maji maarufu kwa jina la “Amanzi App” amesema mfumo huo utasaidia kupunguza upotevu wa maji unaosababishwa na kupasuka kwa mabomba ya maji kutoka asilimia 42 kwa  mwezi hadi kufikia asilimia 21.


Kilangi amesema mamlaka yake ndio yakwanza nchini kuja na mfumo huo ambao utasaidia kutatua changamoto ya upasukaji wa mabomba ya maji na kutatua changamoto hiyo pamoja na kutoa taarifa za wizi wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji kwa kwa manispaa ya Kigoma Ujiji na vitongoji vyake.

Akizungumzia  utendaji kazi wa mfumo huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Collection Tech, Fredrick Swai amesema mfumo huo unafanya kazi kwa urahisi kwa kupakua mfumo “app” hiyo kwenye simu janja (smartphone) na kupiga picha eneo ambalo bomba limepasuka na mfumo huo utachagua fundi aliyepo karibu na atapokea ujumbe kupitia simu yake ya mkononi.

Akizindua mpango huo  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, alisema kuwa uzinduzi wa Amanzi App ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za maji na kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu haipotei ambapo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji  na Mamlaka nyingine za maji mkoani humo  kutumia teknolojia hiyo kama suluhisho la tatizo la upotevu wa maji unaosababishwa na mivujo.

Mkuu huyo wa mkoa Kigoma pia  ametoa wito kwa waendesha pikipiki za abiria (bodaboda) kutumia nafasi yao ya kufika maeneo mbalimbali kuchangia katika kukusanya taarifa za mivujo kwa kutumia App hiyo, hivyo kusaidia serikali kuokoa fedha zinazotumika katika uzalishaji wa maji.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI