Header Ads Widget

ULEGA: WAKANDARASI WAZEMBE IMETOSHA

 

Na Matukio Daima App.

LINDI.WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema serikali haitaongeza hata siku moja kwa mkandarasi ambaye atabainika ameshindwa kukamilisha mradi wa ujenzi aliopewa na serikali kwa sababu za uzembe.

Ulega aliyasema hayo mkoani Lindi akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa ukarabati wa miundombinu ya ujenzi katika mikoa ya Kusini kufuatia maelekezo aliyopewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya mvua kubwa zilizonyesha mwaka huu kuharibu barabara.

Alisema wakati mzuri wa kumaliza kazi za wakandarasi ni huu kabla ya kuanza kwa mvua za vuli na kwamba hatarajii wananchi kuteseka tena wakati wa mvua hizo kwa sababu ya uzembe wa waliopewa kazi ya kujenga barabara na madaraja.

“Serikali imewaamini na kuwapa kazi ya ujenzi wa barabara na madaraja ya kudumu, hakikisheni mnakamilisha kwa ubora na wakati na hatutakubali kuona tena wananchi wakiteseka kama ilivyotokea mwaka jana na mwaka huu,” alisisitiza.

Katika ziara yake hiyo ya ukaguzi, Ulega aliwasilisha pia salamu maalumu za upendo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi ambako kwa sasa, serikali yake inaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa takribani 13 inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Mbunge huyo wa Mkuranga aliwataka wakandarasi wanaojenga madaraja na barabara unganishi mkoani Lindi kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili ikamilike mapema Septemba kabla ya kuanza kwa mvua za vuli.

Ujenzi unaoendelea sasa ni katika barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini kutokana na athari za mvua za El Nino na kimbunga Hidaya ambavyo kwa pamoja vilisababisha kukatika kwa barabara za Marendego Nangurukuru-Lindi-Mingoyo, Kiranjeranje-Namichiga, Tingi-Kipatimo, Nangurukuru-Liwale na Liwale-Nachingwea.

Ili kuhakikisha kazi ya ujenzi inakwenda kwa kasi, Ulega aliwataka wakandarasi kuongeza idadi ya wafanyakazi na muda wa kufanya kazi bila kujali usiku na mchana, ili kazi iende kwa kasi na pia kusaidia vijana kupata riziki.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI