Na Matukio Daima App.
DODOMA: UJENZI wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma maarufu kwa jina la Ring Road umefikia zaidi ya asilimia 85 ya utekelezaji wake.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amepewa taarifa hiyo leo wakati alipokuwa akifanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 112.3 ni miongoni mwa barabara za kimkakati mkoani Dodoma na katika ziara yake ya ukaguzi wa barabara hiyo jana, Ulega aliwaambia wana habari kwamba barabara hiyo itaung'arisha mji huo hasa nyakati za usiku kwani itafungwa taa za barabarani njia nzima.
"Nimekagua na nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika awamu zote mbili na malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na nimeelekeza wataalam kutoka TANROADS hadi kufikia mwezi Juni ujenzi uwe umefikia asilimia 90", amesisitiza Ulega.
Ulega alisema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu tu ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika jiji la Dodoma na Tanzania kwa ujumla chini ya Rais Samia na waziri huyo ametumia ziara yake hiyo kutangaza kuwa serikali inatarajia kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji hilo ambapo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga mradi huo.
Alisema katika eneo la Ihumwa, serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kisasa ya njia za kupishana (interchange), ili kuruhusu magari kupita katika mji wa Serikali wa Magufuli na yaendayo mjini bila kuwa na kizuizi chochote.
0 Comments