Uingereza, Ufaransa na Canada zimeionya Israel kuwa zitachukua "hatua madhubuti" ikiwa itaendelea na upanuzi "mbaya" wa operesheni za kijeshi huko Gaza.
Sir Keir Starmer aliungana na viongozi wa Ufaransa na Canada kuitaka serikali ya Israel "kukomesha operesheni zake za kijeshi" na "kuruhusu mara moja msaada wa kibinadamu kuingia Gaza".
Hakuna chakula, mafuta au dawa iliyoruhusiwa kuingia Gaza tangu tarehe 2 Machi, hali ambayo Umoja wa Mataifa ilieleza hapo awali kama "kusababisha maafa" kwa wakazi wa Palestina.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alijibu kwa kusema viongozi hao watatu wametoa "tuzo kubwa" kwa Hamas katika vita vya Gaza.
Siku ya Jumapili, Netanyahu alisema nchi yake itaruhusu "kiasi cha chakula" kuingia katika eneo hilo baada ya kizuizi cha muda mrefu cha wiki 11 lakini inapanga "kudhibiti Gaza yote".
Viongozi hao watatu wa Magharibi walikosoa hili kama jambo ambalo si la "kutosheleza kabisa" kwani "kunyimwa msaada muhimu wa kibinadamu kwa raia ni jambo lisilokubalika na kuna hatari ya kukiuka Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu".
0 Comments