Header Ads Widget

TUNASIMAMA NA RAIS SAMIA KUPINGA WANAOKUJA KUVURUGA AMANI YETU – ISLAM HUWEL


NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

MJUMBE wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM ) Taifa anayewakilisha wilaya ya Iringa mjini Islam Huwel amesema Taifa letu Tanzania limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na utulivu wake, hasa kupitia kauli na hatua thabiti zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo kila mtanzania anampongeza

 kuwa siku tatu zilizopita, Rais Samia alitoa onyo kali kwa baadhi ya wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania kwa namna inayoweza kuhatarisha utulivu wa kitaifa. 

Alisema kuwa onyo hilo limeungwa mkono na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na wao kama viongozi na wana CCM wanaunga mkono na kumpongeza sana  Rais Samia kwa msimamo wake madhubuti.

Akizungumza na Matukio Daima Media Huwel alisema kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utulivu, na kwamba ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha anasimama imara kulinda hali hiyo. 

kuwa baadhi ya mataifa duniani yamekumbwa na misukosuko ya kisiasa na kijamii, hivyo ni rahisi kwa baadhi ya watu kutoka nchi hizo kutamani kuona hali kama hiyo ikitokea pia Tanzania. 


“Tanzania yetu ni nchi ya utulivu na amani, hatupaswi kuruhusu wageni kuja kutuvuruga ni jukumu letu kama Watanzania kuilinda amani yetu,” alisema Huwel.

Akitolea mfano hali ya baadhi ya nchi jirani, Huwel alisema kuna baadhi ya mataifa ambayo amani ni hadithi ya zamani, na badala ya kutatua changamoto zao, wanajaribu kueneza machafuko kwa wengine. 

Kuwa wakati huu ambao taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu, ni kipindi kinachohitaji umakini mkubwa kwani chokochoko mbalimbali huibuka, nyingi zikiwa zimechochewa na watu kutoka nje wanaotafuta faida binafsi au kutimiza malengo ya kisiasa yasiyo na maslahi kwa Watanzania.


Katika hatua nyingine, Waziri Kiongozi wa Kenya, Musalia Mudavadi, ameungana na Rais Samia katika kukemea mienendo ya wanaharakati wa kigeni wanaokuja Tanzania kwa sababu zisizo rasmi. 

Katika mahojiano na kituo cha runinga cha Citizen TV cha nchini Kenya, Mudavadi alisema kuwa hawezi kupinga kauli ya Rais Samia kwa sababu ina ukweli mkubwa ndani yake. 

“Huko kwetu Kenya, uhuru wa maoni umevuka mipaka hatuwezi tena kuzungumza kwa heshima Kauli ya Rais Samia ina msingi mzuri na ni ya kuungwa mkono,” alisema Mudavadi.

Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Samia alifichua kuwa baadhi ya wanaharakati hao walitokea Kenya, na walikuja nchini kwa kisingizio cha kufuatilia kesi ya mwanasiasa wa upinzani, Tundu Lissu. 

Hata hivyo, Rais alieleza kuwa lengo la wanaharakati hao halikuwa kufuatilia kesi hiyo kwa nia njema, bali kulikuwepo na dhamira ya kuchochea vurugu na kuharibu hali ya amani ya nchi. 

“Walishavuruga kwao, tusikubali waje kutuharibia huku. Tanzania ndiyo nchi iliyobaki salama na yenye utulivu, lazima tuilinde,” alisema kwa msisitizo Rais Samia.

Kauli hiyo ya Rais imepokelewa kwa uzito mkubwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali, ikiwa ni ishara ya ujasiri na dhamira ya dhati ya kulinda heshima na uhuru wa taifa. 

Serikali ya Tanzania imetoa taarifa rasmi ikisisitiza kuwa haitavumilia jaribio lolote la kuchochea vurugu kwa kivuli cha harakati za kijamii au haki za binadamu. 

Katika taarifa hiyo, serikali imesema wazi kuwa Tanzania si uwanja wa majaribio ya kisiasa au vurugu zisizo na msingi, na kwamba nchi itaendelea kuwa ya watu wastaarabu, wanaothamini amani, utu na mshikamano wa kitaifa.

“Tanzania si uwanja wa majaribio ya fujo na siasa za matusi. Serikali iko imara kulinda amani, utu na hadhi ya nchi yetu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Samia, imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kuendeleza diplomasia ya amani, kuimarisha taasisi za umma na kuhimiza utawala wa sheria. 

Viongozi wengi wa ndani wameeleza kuwa siyo tu Rais Samia anatoa tahadhari, bali pia anatekeleza kwa vitendo mikakati ya kuhakikisha kila Mtanzania anaishi katika nchi yenye amani ya kweli.

Islam Huwel alisisitiza kuwa huu ni wakati wa Watanzania wote kusimama pamoja, bila kujali tofauti zao za kisiasa, kidini au kikabila, na kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kulinda na kuendeleza amani ya taifa. 

Alisema kuwa watu wote wenye nia njema wanakaribishwa kushirikiana na Watanzania, lakini ni lazima waheshimu sheria na tamaduni za nchi.

Katika mazungumzo yake, alisisitiza kuwa uvunjifu wa amani una gharama kubwa sana, na mara nyingi huchochewa na watu ambao hawapendi maendeleo ya wengine.

 Hivyo, aliwataka wananchi kuwa macho dhidi ya watu wa aina hiyo, na kuhakikisha wanatoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapohisi kuwepo kwa dalili za uchochezi.

Kwa ujumla, msimamo wa Rais Samia umeonekana kuwa ni sauti ya uzalendo, inayotetea uhuru na hadhi ya Tanzania kama taifa huru na linalojitegemea. 

Wito umetolewa kwa Watanzania wote kutobweteka na hali ya amani iliyopo, bali waendelee kuilinda na kuitunza kwa vitendo.

Katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kisiasa na kijamii, Tanzania inajitokeza kama kisiwa cha matumaini – nchi inayothamini mshikamano, heshima, na maendeleo ya watu wake. 

Ni wajibu wa kila raia kuhakikisha kuwa hali hiyo inaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI