Header Ads Widget

TMA YATOA MWENENDO WA HALI YA HEWA KWA MSIMU WA JUNE - AUGUST, 2025


Na Fatma Ally Matukio DaimaApp 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo imetoa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua kwa kipindi cha Juni hadi Agosti 2025 (msimu wa Kipupwe).

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chan’ga,

ametoa tahadhari na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema kuwa, mwezi Julai ndio kipindi cha baridi zaidi, huku maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuka chini ya nyuzi joto 6°C, hasa katika nyanda za juu kusini-magharibi.

Kwa mujibu wa TMA, msimu wa June/August 2025 utatawaliwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi katika maeneo mengi ya nchi, hata hivyo, baridi kali inatarajiwa hususani katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida na magharibi mwa Dodoma.

Hata hivyo, kutakua upepo wa wastani kutoka Kusini Mashariki utakaotawala maeneo mengi, huku vipindi vya upepo mkali kutoka kusini (upepo wa kusi) vikitarajiwa hususan mwezi Juni na Julai, hasa katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya nchi kavu.

"Ingawa kwa kawaida Kipupwe huwa na ukavu, msimu huu vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara), pamoja na ukanda wa pwani na visiwa vya Unguja na Pemba".

TMA imeeleza kuwa baridi inaweza kupelekea ongezeko la magonjwa ya kuambukiza kama homa ya mapafu, na magonjwa ya mifugo katika baadhi ya maeneo. Pia, vumbi linalosababishwa na upepo linaweza kuathiri afya ya macho na kuongeza hatari ya magonjwa mengine.

Dkt. Chan’ga amewashauri wananchi kuchukua tahadhari za kiafya, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata baridi kali na vumbi, wafugaji wanashauriwa kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo na kufuata ushauri wa wataalamu, huku wakulima wakihimizwa kutumia maeneo oevu kwa kilimo cha mazao ya muda mfupi kama mbogamboga na viazi.

Sambamba na hayo, watumiaji wa shughuli za baharini wametakiwal kufuatilia utabiri wa kila siku na angalizo kuhusu upepo mkali kwa usalama wao.

Kwa mujibu wa TMA, joto la bahari linatarajiwa kuwa la wastani katika maeneo mengi ya tropiki, huku joto la juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi likitarajiwa kudhoofisha upepo wa baridi kutoka kusini.

TMA itaendelea kufuatilia hali ya hewa na kutoa taarifa za mara kwa mara. Wananchi na wadau wanahimizwa kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi kutoka TMA pamoja na tahadhari zinazotolewa kuhusu hali mbaya ya hewa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI