Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt,Jabiri Bakari, amesema kuwa Tanzania inazidi kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kidijitali, kufuatia ongezeko la haraka la laini za simu na watumiaji wa intaneti kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari jijini Dodoma, Dkt,Jabiri amesema Kama waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa alivyosema hadi kufikia Aprili 2025, laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka hadi milioni 90.4 kutoka milioni 73.5 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.9.
Kadhalika, amesema watumiaji wa intaneti wameongezeka kwa asilimia 32.3, kutoka milioni 37.3 hadi milioni 49.3. Hii inaonesha namna Watanzania wanavyokumbatia teknolojia na kuitumia katika maisha yao ya kila siku.
Amesema mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwenye miundombinu ya mawasiliano, hasa minara ya simu ambayo imeongezeka kwa kasi kubwa katika maeneo ya mijini na vijijini.
Ameeleza kuwa Tupo katika zama za uchumi wa kidijitali uchumi unaotegemea teknolojia ya mawasiliano na matumizi ya mitandao katika kila nyanja ya maisha yetu ya kila siku alitahadharisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, kumekuwa na ongezeko la uhalifu wa kimtandao, jambo linalohitaji hatua za haraka.
“Uhalifu umehamia mtandaoni. Tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi na kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha mitandao yetu inabaki salama. Tunawasihi wananchi kuchukua tahadhari wanapotumia mitandao ya kijamii na kufanya miamala ya kidijitali,” aliongeza.
Kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kunatarajiwa kuimarisha zaidi sekta ya mawasiliano, kuongeza kasi ya mabadiliko ya kidijitali na kusaidia kufikia lengo la taifa la kuwa na uchumi wa kidijitali uliojikita katika maarifa, ubunifu na usalama wa kimtandao.
0 Comments