Header Ads Widget

WATUMIAJI WA BARABARA YA NJOMBE -RUVUMA WALIA NA UBOVU

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

Watumiaji wa vyombo vya usafiri wanaopita katika barabara kuu kutoka Makambako kwenda mkoa wa Ruvuma wameitaka Serikali kuifanyia matengenezo upya barabara hiyo kwa kuwa kwa sasa haikidhi viwango kupitisha aina zote za magari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MATUKIO DAIMA MEDIA  baadhi ya wadau hao walisema kuwa barabara ya lami kuanzia Makambako hadi mkoani Ruvuma kwa sasa ni mbaya haifai kupitisha vyombo vya usafiri.

"Barabara hii kiukweli imeharibika kupindukia, malori ya mizigo, mabasi na magari aina zote ni tabu kupita njia hii", alisema Kabeya Muteba dereva wa Lori linalobeba makaa ya mawe huko Mbinga.

Muteba alisema kuwa kwa sasa barabara hiyo ni nyembamba, imeharibika kwa kuwa na mashimo na kuwa ni hatari kwa kupitisha aina zote za magari.

Kauturi Lukamba dereva wa Lori linalofanya safari kutoka Dar es Salaam kwenda kubeba makaa ya mawe huko Mbinga alisema barabara hiyo kutoka Makambako hadi mkoani Ruvuma unaweza kusafiri hata siku mbili hadi tatu kutokana na hali ya ubovu wa barabara hiyo.

"Mimi natoka Dar es Salaam hadi Makambako kwa siku moja, lakini ninapoanza kwenda Ruvuma kuanzia Makambako huwa naumia sana na safari kutokana na ubovu wa barabara hiyo", alisema  Lukamba.

Wananchi wa maeneo ambayo barabara hiyo inapita wamemtaka Waziri wa Ujenzi hapa nchini kufanya mipango ya haraka kuitengeneza barabara hiyo kwa kuifumua na kuitanua ili iweze kukidhi vigezo vya sasa vya usafiri na usafirishaji.

"Yaani mimi nashangaa sana barabara ya muhimu kama hii inatelekezaa kama mtoto wa kambo, kwani sisi wa huku kusini siyo Watanzania, alisema Ibrahim Lwambano kwa masikitiko.

Barabara hiyo ambayo inapita kwenye miteremko mikali, miinuko ya ghafla na ina kona nyingi ingefaa kwa sasa ipanuliwe na kitengenezwa kwa manufaa ya kukuza uchumi wa wananchi na Serikali kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI