Header Ads Widget

SIFACU YATOA OMBI KWA SERIKALI YA SINGIDA ISADIE MALI ZAO ZIREJESHWE

 Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mkoa wa Singida (SIFACU) kimemuomba Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, aingilie kati ili kiweze kurejeshewa mali zake ambazo zipo kwenye mamlaka za serikali za vijjiji na watu binafsi kwa miaka mingi.

Ombi hilo liliwasilishwa jana Mwenyekiti wa SIFACU, Clement Mkumbo,  kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego, wakati wa mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

"Miaka ya 1970 ushirika ulipoyumba nchini sehemu kubwa ya mali za wanaushirika zilikabidhiwa katika mamlaka za serikali kwa ajili ya usimamizi na uangalizi na sisi wanaushirika ni miongoni mwa vyama ambavyo mali zetu zipo kwa wasimamizi wa mamlaka za vijiji na umiliki wa watu binafsi," alisema Mkumbo.

Mkumbo alisema wamefanya jitihada za awali kwa kuunda tume maalum ili kuweza kurahisisha jambo hilo na mali kurejeshwa lakini kumekuwa na changamoto nyingi kutoka kwenye mamlaka za serikali za vijiji na umiliki wa watu binafsi.

"Kupitia hadhira hii wanaushwa Mkoa wa Singida tunakuomba sana mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo yako na msaada wako tunaamini tutafikia hatua nzuri katika urejeshaji wa mali za wanaushirika,"alisema Mkumbo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dendego, akijibu ombi aliagiza mali zote za ushirika ambazo zipo kwenye mamlaka mbalimbali zirejeshwe haraka.

"Kuna mali nyingi za ushirika ambazo zipo nje kwa baadhi ya wanaushirika au katika mamlaka mbalimbali naagizazirejeshwe haraka kwa wanaushirika kama waraka uliotolewa na serikali ulivyoelekeza,"alisema Dendego.

Aidha,Dendego alisema hatawavumilia watu wanaobeba maslahi binafsi kwenye vyama vya ushirika na kuacha maslahi ya wengi kwa kuwa hali hiyo ndio inaufanya ushirika usiweze kuwa na maendeleo yenye kuwanufaisha wakulima.

"Nilikuwa nasoma taarufa zenu za miaka minne ya nyuma mna hati chafu kwenye vyama vyenu, hati chafu maana yake kuna watu wanakula bila kunawa, anzeni kusafisha nyumba zenu kabla mimi sijaja na fagio langu gumu kwenye hili sitanii," alisema Dendego.

Dendego alisema ndoto ya serikali ni kuona kunakuwa na ushirika wenye nguvu ya kimtaji,miundombinu imara,wanachama wengi ambao watakuwa wanawezeshwa kiuchumi na hili linawezekana iwapo kutakuwa na viongozi imara wanaotanguliza maslahi ya wengi.

Alisema katika Mkoa wa Singida ushirika bado haujasimama imara licha ya juhudi zinazofanywa na serikali ambapo kuna vyama vichache,mitaji midogo na pia kuna uchache wa kufikiri.

"Tulikwenda kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani watu wachache wasiozidi 30 walibeba mabango wakawa na nguvu kutaka kuzuia wakulima wasiuze mazao yao kupitia mfumo huo nilitegemea watu wale wangejibiwa na wanaushirika kwa kufanya maandamano kwamba hamuwatambui lakini mkawa wanyonge mnasubiri Mkuu wa Mkoa atafanya nini," alisema.

Mkuu wa Mkoa alisema suala la vyama vya ushirika kuanzisha viwanda vyake haliepukiki kwani serikali inataka kuona wanaushirika wanamiliki viwanda vikubwa kwa ajili ya bidhaa zao wanazozizalisha zinaongezewa thamani.

Naye Katibu Tawala Mkoa waSingida  Dk.Fatuma Mganga alisema asilimia 95 ya wakulima wa mkoa huu wameshasajiliwa kwenye daftari la pembejeo na hivyo wakulima wote wanasifa za kupata pembejeo hizo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI