Na Moses Ng’wat, Mbozi.
Wakazi wa Kijiji cha Namlonga kilichopo Kata ya Nanyala, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, wamepata afueni kubwa baada ya kuanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa uchimbaji wa kisima kilichotekelezwa chini ya Programu ya Visima 900 ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 120 na umewezesha wakazi 870 wa kijiji hicho kuondokana na changamoto ya muda mrefu ya kuchota maji katika Mto Ivanga, maji ambayo walikuwa wakiyatumia pamoja na mifugo yao hali iliyosababisha ongezeko la magonjwa ya tumbo .
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mei 6, 2025, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Mponelo Mwamkinga, alisema maji ya mto waliyokuwa wakiyatumia awali yalikuwa na harufu ya kinyesi cha ng’ombe kutokana na kutumika pia na mifugo.
Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea mradi huu. Sasa tunapata maji karibu na makazi yetu na tumeondokana na adha ya kuamka alfajiri kwenda kuchota maji kwenye makorongo ambayo si salama kwa afya,” alisema Mwamkinga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Meshaki Gunza, alisema mradi huo ni utekelezaji wa dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama, na kuongeza kuwa mradi huo pia utapunguza migogoro ya kifamilia iliyokuwa ikitokana na upatikanaji wa maji.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Ismail Ismail, alisema thamani ya mradi huo ni zaidi ya shilingi milioni 120 na umehusisha uchimbaji wa kisima, ununuzi wa tenki la kuhifadhia maji, na ujenzi wa nyumba ya mitambo ya kusukuma maji.
Alisema mradi huo umewezesha upatikanaji wa huduma kwa wakazi zaidi ya 870 na kwamba Wilaya ya Mbozi imenufaika na jumla ya visima 10 kupitia program hiyo, ambapo baadhi ya miradi ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji huku mingine ikiwa tayari imeanza kutoa huduma.
0 Comments