Na Hamid Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma
WAZIRI wa Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa kutambua mchango wao kama sehemu ya nguvu kazi ya taifa, huku ikiendelea kutekeleza mikakati ya kuwawezesha kijamii na kiuchumi.
Ameyasema hayo leo Mei 9,2025 kwenye mkutano wa Kitaifa wa mashauriano uliolenga Mgao wa 30% za Samia kupitia NeST mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na Matumizi ya Mfumo wa NeST Kwa watu wenye mahitaji maalum na kujadili haki na ustawi wa watu wenye ulemavu
Aidha amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia vikundi vya watu wenye ulemavu, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wanajitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
“Ni wajibu wangu mimi na viongozi wenzangu kuhakikisha tunasimamia vyema masuala ya watu wenye ulemavu, kwani fedha zimeendelea kupelekwa kwa vikundi vyao ili kuleta tija katika maisha yao,” amesema Ridhiwani.
Aidha, Serikali inaendelea kujenga shule jumuishi kwa wanafunzi wenye ulemavu nchi nzima, sambamba na kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ili iendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya elimu jumuishi.
Katika hatua nyingine, Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za mafuta ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanapatiwa mafuta maalum bure, kama njia ya kukabiliana na changamoto ya saratani ya ngozi.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Winfrida Samba, amesema kuwa mfumo wa NeST umeendelea kuwa fursa muhimu kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa umewawezesha kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa manunuzi ya umma.
Amesema mfumo huo umefanikisha usajili wa jumla ya watu 1,335 wenye ulemavu katika kanzidata ya wazabuni, hatua ambayo si tu imeongeza uwazi na ushirikishwaji, bali pia imewapa nafasi ya kushindana kwa haki kwenye zabuni mbalimbali serikalini.
Amesisitiza kuwa PPRA itaendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu ili kuhakikisha wanaitumia ipasavyo mifumo ya kisasa inayowezesha ushiriki wao katika uchumi wa taifa.
Awali akisoma risala Muasisi wa Ikupa Trust Fund Stella Ikupa, amesema kuwa licha ya juhudi za Serikali kuboresha huduma za afya, bado watu wenye ulemavu wanakumbwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa saidizi, miundombinu isiyokuwa rafiki, na uhaba wa watumishi wa afya waliopata mafunzo ya kuwahudumia kikamilifu.
Kutokana na hayo Ikupa ameiomba Serikali kuzingatia kwa makini mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu wakati wa utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma katika upatikanaji wa huduma bora za afya.
"Changamoto ya upatikanaji wa huduma zimekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wenye ulemavu katika kufurahia haki zetu za msingi ya kupata huduma bora za afya, "
"Tunapojadili bima ya afya kwa wote, lazima tuhakikishe kuwa tunawaangalia watu wenye ulemavu kwa jicho la kipekee, kwa sababu mahitaji yao si sawa na ya watu wengine," amesema Ikupa.
Aidha, akagusia kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu, ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika mchakato mzima wa siasa na demokrasia.
Ametoa wito kwa vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi na vyombo vya habari kuhakikisha kunakuwepo na wakalimani wa lugha ya alama katika kampeni, mikutano ya hadhara na matangazo ya moja kwa moja ya kisiasa kupitia televisheni na majukwaa mengine ya habari.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata taarifa sawa kama wananchi wengine. Hii ni sehemu ya haki ya kupata habari, ambayo ni msingi wa ushiriki kamili katika shughuli za kijamii na kisiasa,” amesisitiza.
Kwa upande mwingine, Ikupa amelipongeza shirika lake lililoandaa mkutano huo kwa udhamini wa PPRA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapatiwa mahitaji yao muhimu, ikiwemo misaada ya vifaa saidizi, mafunzo ya kujitegemea, na elimu ya haki zao.
“Shirika hili limekuwa likifanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linapaza sauti na linapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa letu,” amesema.
Aidha ameishukuru Serikali kupitia PPRA kwa kutenga asilimia 30% ili makundi maalum yaweze kunufaika na mchakato wa manunuzi ya Umma.
Mwisho.
0 Comments