Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nchi jirani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo haliwezi kuwa “shamba la bibi” ambapo kila mtu anaingia na kufanya apendavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), Rais Samia amesema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.
“Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku,” alisema Rais Samia.
Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, pamoja na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na wanaharakati wengine wawili, kuzuiwa kuingia nchini Tanzania.
Walikuwa wamewasili kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu, ambayo imeendelea leo katika Mahakama ya Kisutu.
Kwa mujibu wa Karua, alifurushwa na kurudishwa Kenya kwa lengo la kumzuia kuhudhuria kesi hiyo. Mutunga na wenzake pia walielezwa kuwa walizuiwa katika uwanja wa ndege kabla ya kurejeshwa nchini kwao.
Hadi sasa, maafisa wa serikali ya Tanzania hawajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, kauli ya Rais Samia imeonekana kutoa mwelekeo wa msimamo wa serikali juu ya suala hilo.
"Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu, aliongeza Rais Samia.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Korir Sing’oei, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu na ushirikiano wa kikanda.
Karua, anayefahamika kwa kusimama kidete kwa haki za binadamu, amewahi kumwakilisha kiongozi wa upinzani Uganda, Kizza Besigye, katika kesi kama hizi, na amekuwa mkosoaji mkubwa wa kile anachokiita kurudi nyuma kwa demokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wasimamizi wa sera za nje, wanapaswa kuhakikisha kuwa hakuna “watovu wa adabu” kutoka mataifa mengine wanaovuka mipaka ya Tanzania na kuingilia masuala ya kitaifa.
“Niombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na ninyi wasimamizi wa sera zetu za nje, msitoe nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kuvuka hapa kwetu,” alisisitiza.
Kesi ya Tundu Lissu inaendelea huku mashinikizo kutoka ndani na nje ya nchi yakiongezeka, yakihusisha madai ya ukandamizaji wa haki za kiraia na kisiasa, jambo ambalo Serikali ya Tanzania inakanusha.
0 Comments