Header Ads Widget

PROF MKENDA: MABADILIKO YA MITAALA NGUZO MUHIMU YA KUHIMARISHA ELIMU NCHINI

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

WAZIRI  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu kupitia maboresho makubwa ya mitaala katika ngazi zote za elimu nchini.

 Maboresho hayo, yanalenga kuongeza ujuzi, maarifa na stadi za wanafunzi, ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuhakikisha elimu inakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO wakati akieleza mafanikio ya Serikali ya wamu ya sita Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali imeanzisha mikondo miwili ya elimu ya Sekondari, Mkondo wa Jumla na Mkondo wa Amali, pamoja na kuweka mfumo wa elimu kuwa nyumbufu, ili kuhakikisha wanapokea ujuzi na maarifa yanayozingatia mahitaji halisi ya taifa na soko la ajira.

“Tumeweka somo la lazima la elimu ya Biashara na Historia ya Tanzania, huku tukiboresha mifumo ya ufundishaji lugha ili kuongeza ufanisi wa ujifunzaji,” amesema Waziri Mkenda.

Aidha, amebainisha kuwa mitaala 389 katika elimu ya ufundi na mitaala 563 katika elimu ya juu imeboreshwa ili kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na kuzingatia stadi za karne ya ishirini na mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Waziri Mkenda pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Elimu (Sura 353) ili kuendana na mabadiliko haya ya sera na mitaala.

 “Tunaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kuhakikisha Sheria yetu inakidhi mahitaji ya sasa,” amesema.

Aidha, Serikali imehuisha miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Taifa wa Tuzo na Sifa Linganifu za Kitaaluma (TQF), Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule, Mwongozo wa Utambuzi wa Vipawa na Vipaji, pamoja na Mwongozo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.

Pia, Waziri Mkenda ametangaza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika elimu, ikijumuisha miongozo ya matumizi ya teknolojia katika shule, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, pamoja na matumizi ya Akili Bandia (Artificial Intelligence) kwa mwaka 2025.

Amesema Serikali imeandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Ujifunzaji unaolenga kurahisisha upimaji wa wanafunzi katika shule za msingi na kuimarisha huduma kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Katika sekta ya elimu ya juu, Waziri Mkenda amesema Serikali imeanza ujenzi wa majengo ya madarasa, maabara na mabweni katika kampasi kuu na za pembezoni katika mikoa 16 ambayo haikuwa na taasisi za elimu ya juu. 

Mradi huo wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye thamani ya shilingi bilioni 972, utaongeza uwezo wa taasisi hizi katika kudahili wanafunzi zaidi na kupunguza uhaba wa wahadhiri kwa asilimia 20.

“Tunahakikisha kwamba elimu yetu inazalisha wataalamu wenye ujuzi na stadi zinazohitajiwa katika soko la ajira ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” alisisitiza Waziri Mkenda.

Waziri amewataka wananchi na wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mfumo wa elimu nchini.

"Kwa taarifa zaidi, wananchi wanaweza kutembelea tovuti rasmi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia: www.moe.go.tz. , " amesema


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI