Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limepokea msaada wa pikipiki mbili aina ya Boxer kutoka kwa kampuni ya TAZAMA Pipeline, ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika jijini Mbeya, Mkuu wa Rasilimali Watu wa TAZAMA Pipeline, Ndugu Greatus Nsemwa alisema kuwa kampuni hiyo imeguswa na jitihada kubwa zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha usalama wa wananchi, hivyo kuona umuhimu wa kutoa msaada huo ili kuongeza ufanisi wa kazi.
“Jeshi la Polisi ni wadau wakuu wa masuala ya ulinzi na usalama nchini. Kama TAZAMA Pipeline, tumeona ni wajibu wetu kutoa mchango huu mdogo lakini wenye lengo la kuongeza nguvu katika juhudi za kulinda maisha na mali za wananchi,” alisema Nsemwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo muhimu na kuahidi kuwa pikipiki hizo zitatumika ipasavyo katika kuimarisha doria na kusaidia askari kufika kwa haraka katika maeneo mbalimbali ya kazi.
“Pikipiki hizi zitasaidia kuongeza kasi ya majibu kwa matukio ya dharura na kuimarisha doria hasa katika maeneo ambayo magari hayawezi kufika kwa urahisi,” alisema SACP Kuzaga.
Aidha, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu wa Polisi (SP) Notker Kilewa alieleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha usalama barabarani, ikiwemo kupishanisha magari makubwa na madogo katika maeneo hatarishi kama Mlima Iwambi na Inyala, ili kupunguza athari za ajali.
SP Kilewa aliongeza kuwa Jeshi hilo linaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kufungia leseni, kutoza faini na kuwafikisha mahakamani, ikiwa ni juhudi za kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.
0 Comments