NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa imekamata magari 230 yanayotumia barabara za umma bila bima katika ukaguzi wa siku tisa uliofanyika wilayani Nyamagana, Ilemela, na Misungwi mkoani Mwanza.
Zoezi hili linalenga kuhakikisha wamiliki wa magari wanafuata Sheria ya Bima ya Vyombo vya Moto ya mwaka 2009 (Sura 169) na kuwalinda dhidi ya hasara zinazoweza kutokea barabarani.
Jumla ya magari 2,170 yalikaguliwa, na kati ya yale 230 yaliyokosa bima, 171 yalitimiza matakwa ya kisheria kwa kukata bima papo hapo, kulingana na Afisa Ubora wa TIRA, Halfani Jumanne.
“Wamiliki wengi wameonesha uwajibikaji kwa kukata bima mara moja, jambo linaloonyesha mafanikio ya zoezi hili,” amesema Jumanne.
Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa, Richard Toyota, ameeleza kuwa lengo la ukaguzi ni kutekeleza sheria inayolazimisha kila chombo cha moto kuwa na bima ya angalau kiwango cha chini.
“Bila bima, dereva anaweza kupata hasara kubwa bila fidia iwapo ajali itatokea, jambo linalowaathiri wao na watumiaji wengine wa barabara,” alisema Toyota.
Aliongeza kuwa TIRA pia inakagua vituo vya mafuta ili kuhakikisha vinakidhi viwango vya bima.Katika zoezi hilo, TIRA ilitoa elimu kwa madereva, makondakta, na wamiliki wa magari kuhusu umuhimu wa bima na jinsi ya kukagua hali ya bima zao kupitia mfumo wa Tiramis.
“Mfumo huu unawaruhusu wamiliki kuthibitisha bima ya vyombo vyao kwa urahisi,” Amefafanua Jumanne
Madereva kama Bakari Said na Mwita Robert waliunga mkono zoezi hilo, wakisema bima inawasaidia kulipa fidia wakati wa majanga kama ajali.
“Bima inalinda maisha yetu na mali zetu na ni muhimu sana kwa Kila mmiliki na dereva kukata bima ili iweze kuwasaidia,” alisema Said.
TIRA inawahimiza wamiliki wa magari Mwanza na maeneo ya jirani kukata bima ili kuepuka adhabu na kulinda usalama wao na wa wengine. Zoezi la ukaguzi litaendelea ili kuhakikisha sheria inatekelezwa kikamilifu.
0 Comments