Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kulipiza kisasi dhidi ya Wahouthi baada ya kombora lililorushwa na kundi hilo kupiga uwanja wa ndege wa Israel.
Katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, Netanyahu alitishia kufanya shambulio akisema: "Tulishambulia siku za nyuma, tutashambulia siku zijazo".
Kombora hilo, lililorushwa kutoka Yemen na kundi linaloungwa mkono na Iran, lilitua karibu na kituo kikuu cha uwanja wa ndege wa Ben Gurion Jumapili asubuhi, mamlaka ya Israel ilisema.
Watu wanne walijeruhiwa na mlipuko huo, na wengine wawili kujeruhiwa wakiwa njiani, vyombo vya habari vya Israel viliripoti, vikitoa huduma za dharura.
Baadaye siku ya Jumapili, Wahouthi walisema wataweka "kizuizi kikubwa cha anga" kwa Israeli kwa kulenga mara kwa mara viwanja vyake vya ndege, kujibu mipango ya jeshi la Israeli ya kupanua operesheni huko Gaza.
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, alijibu shambulio hilo kwa kusema: "Yeyote atakayetupiga, tutampiga mara saba zaidi".
Katika taarifa ya baadaye, Netanyahu alisema "mashambulizi ya Houthi yanatoka Iran", akiongeza Israeli itajibu shambulio la Houthi, na kwa Iran "kwa wakati na mahali tunapochagua".
Picha ambazo hazijathibitishwa zilizochapishwa mtandaoni zilionekana kuwaonesha madereva kwenye barabara iliyo karibu wakisimama ili kujificha huku ndege ikitua, na kusababisha moshi mwingi mweusi karibu na uwanja wa ndege, ulio viungani mwa Tel Aviv.
0 Comments