NA MWANDISHI WETU.
WAKATI siku za Wabunge kuendelea kuwawakilisha wananchi wa majimbo yao Bungeni zikihesabika, joto limezidi kuwa kali kwa baadhi ya Wabunge hao baada ya kuwa na wasiwasi na hatima yao na uhakika wa kurejea Bungeni.
Hatua hii inapelekea baadhi ya Wabunge wasiokubalika katika majimbo yao kwa kutofanya kazi za kuridhisha nakuwa na mahusiano mabaya na wananchi katika miaka mitano tangu walipochaguliwa na sasa kuwatafuta viongozi wa chama kwa gharama kubwa wawabebeshe mzigo wa lawama ili kuona uwezekano wa kuwadanganya tena wananchi wawachaguwe na kurejea mjengoni.
Jimbo la Handeni mjini mkoani Tanga ni jimbo linaloongozwa na Mbunge Reuben Mtahamanilo Kwagilwa (CCM).
Mbunge huyo baada ya kuona hatima yake kuwa ndogo sasa ameanza kumtumia Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni, Amiri Changogo na mwenezi wa wilaya, Mkobe kuwatisha wanachama wote wa chama hicho wenye nia ya kugombea jimbo hilo mwaka huu.
Viongozi hawa wameahidiwa zawadi nono endapo Kwagwilwa atarudi bungeni.
Akitoa taarifa kwa masikitiko makubwa, Mmoja wa rafiki wa karibu zaidi na Mbunge huyo ambae ni Diwani katika Halmashauri ya Mji Handeni, amesema ni kweli Mbunge amekuwa akimtumia Mwenyekiti wa CCM kuwatisha viongozi wa kata ,matawi na wajumbe kwa ujumla.
Alisema kuwa, Mwenyekiti ndio mwenye kauli ya mwisho yaani mtu wa mwisho kusema katika chama ambapo Wajumbe wamekuwa wakimshangaa sana Mwenyekiti wao huyo kuwa mtu tofauti na alivyokuwa awali.
Mmoja wa wanachama wa CCM kutoka kata ya Chanika alisikika akisema “Sisi wanachama wa CCM ambao tuna nia ya kugombea katika jimbo la Handeni mjini hatuna amani kabisa kwani Mwenyekiti wa CCM amekuwa akitumika na Mbunge vibaya kututisha endapo tutagombea na ameahidi kuwa atahakikisha tunafukuzwa ndani ya chama kabla ya muda wa uchaguzi ambapo hii ni kinyume na Katiba ya CCM inayomtaka kila mwachama anahaki ya kuchagua na kuchagulia” alisema mwana chama huyo.’’.
Mtoa taarifa ameendelea kudai kuwa, Mbunge amekuwa akimtumia Mwenyekiti huyo nyakati za usiku kuwafuata Wajumbe na kumwombea msamaha Mbunge huyo ambaye ameonyesha kutokuungwa mkono na watu wengi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake, kushindwa kutimiza ahadi zake pamoja na kujikweza baada ya kupewa nafasi hiyo.
Msemaji amesema pia alitumia nafasi hii kuwaomba Viongozi wa CCM ngazi ya Mkoa wa Tanga na Taifa kumuonya Mwenyekiti huyo kuacha kutumika kwa maslahi ya mtu mmoja na badala yake asimame katika nafasi yake na kuwaachia wanachama haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.
“Yani huku kwetu Mwanaccm ukionekana humuungi mkono Mbunge ni kosa utatafutiwa kila aina ya fitina ili kuhakikisha kuwa unamuunga mkono Mh Mbunge au Mwenyekiti wa CCM wilaya akushughulikie hii sio haki kabisa
Alipotafutwa Mwenyekiti huyo kwa njia ya simu alisema kuwa, chama kinautaratibu wa kuwasemea viongozi waliopo madarakani kwani wametumwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi.
Changogo alisema kuwa, viongozi wanapokuwa madarakani wao kama viongozi wa chama wanawajibu wa kuwasapoti na pale wanapomaliza muda wao na Binge kuvunjwa ndio inakuwa kikomo cha kutowasemea.
"Siwatishi wanachama wengine wa CCM wenye nia ya kuchukua fomu pindi muda utakapofika kwani kufanya hivyo ni kukiuwa chama na Handeni kelele ni nyingi na nimeendelea kuvumilia kelele hizo" Alisema Changogo.
Mwisho
0 Comments