Header Ads Widget

MLINZI WA KIONGOZI WA UPINZANI ALIYEPOTEA UGANDA ATUPWA MAHAKAMANI

 Mlinzi mkuu wa Bobi Wine, Edward Sebuufu almaarufu Eddie Mutwe, ambaye alikuwa hajulikani alipo kwa siku kadhaa, ametupwa katika Mahakama Kuu ya mji wa Masaka, kusini mwa Uganda, umbali wa takribani kilomita 130 kutoka mji mkuu Kampala—ambako anatarajiwa kufunguliwa mashtaka.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, aliletwa katika eneo la mahakama na maafisa wa usalama waliowazuia waandishi wa habari kumrekodi au kuripoti kuhusu kesi yake. Hadi sasa haijafahamika mashtaka yatakayomkabili.

Kupitia chapisho la mitandao ya kijamii, kiongozi wa upinzani Bobi Wine alisema kuwa mlinzi wake amepigwa na kuteswa vibaya, na sasa anashikiliwa katika gereza kuu la mji wa Masaka.

Eddie Mutwe ni mlinzi mkuu wa Bobi Wine—msanii wa muziki aliyegeukia siasa na kuwa mpinzani mkubwa wa rais wa muda mrefu nchini Uganda, Yoweri Museveni.

Inaripotiwa kuwa Edward Sebuufu alitekwa Aprili 27 na watu wasiojulikana waliovaa sare za kiraia na za kijeshi, katika mji wa Kiwango katikati mwa Uganda, jambo lililosababisha ghadhabu na hofu kubwa miongoni mwa wananchi.

Baada ya kutoweka kwake, Mkuu wa majeshi ya Uganda na kijana wa Rais Museveni, Muhoozi Kainerugaba, alidai kupitia mitandao ya kijamii kuwa alikuwa akimshikilia kwenye handaki lake.

Aidha, alitoa vitisho vya kutumia nguvu dhidi yake, jambo lililoibua taharuki zaidi.

Wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu wamelaani kushikiliwa kwa Sebuufu na jeshi, huku Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda nayo ikitoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja.

Wakati huohuo, mashirika ya kijamii yameonya kuwa kukamatwa kwake ni sehemu ya kampeni ya kimfumo ya kuwakandamiza wapinzani na kuzima sauti za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka ujao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI