CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, amesema kuwa migogoro ya ndoa imekuwa chanzo kikuu Kwa watoto kujiingiza katika vitendo visivyo na tija kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ngono katika umri mdogo, maambukizi ya virusi vya UKIMWI, na hata watoto kukimbia familia zao na kuwa watoto wa mitaani.
Akizungumza leo Mei 24, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia na Kongamano la Malezi lililofanyika jijini Mwanza, Dkt. Biteko alieleza kuwa lengo la kongamano hilo ni kuthamini nafasi ya familia katika makuzi na malezi ya mtoto, ambao ndio msingi wa jamii bora.
Ameeleza kuwa ni muhimu kuzingatia malezi bora ya mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama hadi anapofikia umri wa miaka 18. Ili kufanikisha hili, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa na kutekeleza Programu Jumuishi za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kipindi cha 2024 hadi 2026.
“Programu hiyo imesaidia kuanzishwa kwa vituo 4,178 vinavyotoa huduma za awali kwa watoto zaidi ya laki nne, huku vituo 206 vinavyomilikiwa na jamii vikihudumia watoto 11,675,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kutenga muda wa kujadili changamoto zao za kifamilia bila kuwahusisha watoto. “Watoto wamekuja duniani sisi tukiwepo, kwa nini tugombane mbele yao? Myamalize nyie wenyewe bila kushirikisha watoto.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2024–2025, Idara ya Ustawi wa Jamii imepokea mashauri 3,534 ya migogoro ya kifamilia, ikiwemo migogoro ya ndoa 980, ambayo imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa watoto wa mitaani.
“Tulifanya uchunguzi kwa zaidi ya watoto 1,000 wa mitaani na sababu kuu walizotaja ni migogoro ya ndoa katika familia zao,” alisema Mtanda.
Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Zainabu Hamis, amesema kuwa malezi ya mtoto yanaanza pindi tu anapozaliwa, hivyo ni jukumu la pamoja la baba na mama kushirikiana katika malezi ili kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri na kupata haki zao zote za msingi.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha utekelezaji wa programu ya malezi bora kwa watoto unasimamiwa kikamilifu na kwa mafanikio.
Maadhimisho haya yamelenga kuimarisha mshikamano wa familia na kuongeza uelewa juu ya nafasi ya wazazi na jamii kwa ujumla katika kulea kizazi bora kitakacholijenga taifa lenye maadili, usawa na maendeleo endelevu.
NA
0 Comments