Tanzania imeandika historia mpya katika uongozi wa afya barani Afrika baada ya Profesa Mohamed Yakub Janabi kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo Mei 18, 2025.
Uchaguzi huo ulifanyika mjini Geneva, ambapo Profesa Janabi alipata kura 32 kati ya 46 zilizopigwa, akiwashinda Mijiyawa (Togo), Dk. N'Da Konan Michel Yao, (Ivory Coast) na Mohamed Lamine Dramé, (Guinea)
Kuchaguliwa kwake kunakuja baada ya kifo cha aliyekuwa amechaguliwa awali, Dkt. Faustine Ndugulile pia kutoka Tanzania, ambaye alifariki ghafla Novemba 2024, muda mfupi kabla ya kuanza rasmi majukumu yake.
Profesa Janabi, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya moyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mshauri wa Rais Samia Suluhu kwenye eneo la afya na daktari wa rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini Tanzania.
Baada ya ushindi huu, jina la Profesa Janabi litathibitishwa na kikao cha 157 cha Bodi ya Utendaji ya WHO, kitakachofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 29 Mei 2025 huko Geneva. Kwa mujibu wa utaratibu Janabi atahudumu kwa kipindi cha miaka mitano lakini anaweza kuteuliwa tena kuhudumu kipindi kingine cha miaka mitano.
Majukumu ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus (katikati) alikuwepo kwenye mchakato ulimchagua Prof Janabi (kulia)
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika ana jukumu la kuongoza na kusimamia shughuli zote za WHO katika nchi 47 wanachama wa kanda hiyo.
Majukumu haya ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kimkakati kwa programu za afya, kuratibu juhudi za kukabiliana na dharura za kiafya kama vile milipuko ya magonjwa, na kuhakikisha usawa katika ugawaji wa rasilimali na huduma za afya katika kanda.
Aidha, Mkurugenzi huyu anapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali, mashirika ya kiraia, na sekta binafsi, katika kuboresha mifumo ya afya, pamoja na kusimamia rasilimali watu na kuhakikisha mafunzo na maendeleo endelevu ya wafanyakazi wa afya.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Kanda pia inawajibika katika kuendesha ajenda ya mabadiliko ya WHO, ambayo inalenga kuboresha utendaji wa shirika hilo kwa kuwa na mwelekeo wa matokeo, ufanisi wa kiufundi, na ushirikiano wa kimkakati.
Yawe majukumu mazito ama mepesi, yaliyo ndani ya uwezo wake ama nje ya uwezo wake, Janabi anaonyesha kujiamini.
"Asanteni kwa kuniamini. Sitawaangusha. Msaada wenu unaonyesha azma yetu ya pamoja ya kujenga Afrika yenye afya bora, imara na yenye mshikamano zaidi," alisema Profesa Janabi baada ya kuchaguliwa.
Changamoto zinamzosubiri Prof. Janabi
Magonjwa ya milipuko na moja ya changamoto kubwa barani Afrika
Profesa Janabi anakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake mapya. Kulingana na ripoti ya WHO, kanda ya Afrika inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi wa afya, hali inayozuia utoaji wa huduma bora za afya. Hii ni changamoto anayopaswa kuishughulikia.
Nchi nyingi za Afrika pia zina mifumo ya afya isiyo imara, jambo linaloathiri uwezo wa kukabiliana na magonjwa na dharura za kiafya. Aidha, mabadiliko ya hali ya hewa yamechangia kuongezeka kwa magonjwa kama malaria, ambapo vifo vinavyotokana na malaria vimeongezeka kwa mwaka wa tano mfululizo.
Hata hivyo wataalamu wa afya barani Afrika wameelezea matarajio yao kwa uongozi mpya wa Profesa Janabi. Katika mahojiano na vyombo vya habari, Dkt. Chikwe Ihekweazu, ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha WHO kinachoshughulika na dharura za kiafya na aliyekua anakaimu nafasi aliyopata Janabi, alieleza kuwa: "Uteuzi wa Profesa Janabi unakuja wakati ambapo Afrika inahitaji uongozi thabiti katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazozidi kuongezeka, ikiwa ni pamoja na milipuko ya magonjwa na mabadiliko ya tabianchi."
Janabi mwenyewe anajua anakwenda kukabiliana na changamoto za aina gani; "Tunapokabili changamoto mbalimbali kuanzia magonjwa ya kuambukiza, yasiyo ya kuambukiza, hadi mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa fedha za afya, ni lazima tutumie uimara na mshikamano wa Kiafrika", anasema Janabi.
Anaeleza na kuhaidi kupitia vipaumbele vyake saba; "Naahidi kusimamia uboreshaji wa huduma za afya kwa wote ili kuweza kufikia malengo endelevu, hadi sasa ni 46% pekee wanapata huduma bora za afya Afrika huku lengo la kidunia ni kufikia 68% mwaka 2030, pili nitasimamia upatikanaji wa rasilimali fedha za kuwezesha kugharamia upatikanaji wa huduma bora za afya".
Matarajio kwa Tanzania na Afrika Mashariki
Waziri wa Afya wa Tanzania Jenista Mhagama, pamoja na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Mazrui, waliongoza ujumbe wa Tanzania huko Geneva
Kulikuwa na kampeni kubwa ya kidiplomasia iliyoongozwa na serikali ya Tanzania, ikiwemo ushawishi wa balozi zake na wadau wa afya katika kanda.
Nchi inajua kwanini impiganie mtaalamu wa aina yake kuwa sehemu ya maamuzi kwenye chombo muhimu na kikubwa kama WHO kwenye eneo la afya.
"Uzoefu wake na utendaji kazi wake pamoja na mafanikio aliyoyapata yanajieleza yenyewe. Nina imani kwamba, uongozi wake utaleta matokeo chanya ya afya na ustawi wa jumla katika bara letu la Afrika," kauli ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania hivi karibuni, kumuunga mkono Profesa Janabi.
Kuchaguliwa kwa Profesa Janabi kwa namna fulani kunatarajiwa kuleta manufaa kwa Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla. Kwa kuwa na Mtanzania katika nafasi ya juu ya uongozi wa WHO Afrika, kuna matarajio ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya WHO na nchi za kanda hii katika maeneo kadhaa.
Moja ya maeneo muhimu ni kuwepo kwa mikakati ya pamoja ya kuboresha mifumo ya afya, ikiwemo mafunzo ya wafanyakazi wa afya na uboreshaji wa miundombinu.
Kuongezeka kwa uwezekano wa kupata ufadhili wa miradi ya afya kutoka kwa wafadhili wa kimataifa kupitia WHO ni jambo linalotazamwa pia. Pamoja na kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazovuka mipaka, kama vile milipuko ya magonjwa.
Kwa ujumla, uteuzi wa Profesa Janabi unatoa fursa kwa Tanzania na Afrika Mashariki kushiriki kikamilifu katika kuunda sera na mikakati ya afya ya kanda, na hivyo kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MWISHO.
0 Comments