📌 Ampongeza Dkt. Tulia kwa ubunifu na kusaidia wahitaji
📌 Wananchi 9,000 wapata bima za afya kupitia Tulia Marathon
📌 Awashukuru wadau na wasanii kwa kushiriki Tulia Marathon
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa mchango wake katika sekta za afya na elimu sambamba na kusaidia wahitaji jijini Mbeya.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Mei 10, 2025 jijini Mbeya mara baada ya kukimbia mbio fupi za Tulia (Tulia Marathon) katika Uwanja wa Sokoine.
“ Dkt. Tulia anafanya kazi kubwa kwenye sekta ya afya na elimu pamoja na kuwajengea nyumba watu wenye uhitaji. Zile nyumba tunazoziona anawakabidhi watu kumbe tayari kuna nyingine zimejengwa Uyole,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Nataka niwaambie hakuna sadaka kubwa kama kusaidia wahitaji na sisi wengine tunajifunza kupitia wewe Dkt. Tulia,”
Ameongeza kuwa Dkt. Tulia ni mtu anayejua kubuni vitu vyenye kuleta matokeo ambapo kupitia tukio la Tulia Marathon amesaidia kutoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali.
Aidha, Dkt. Biteko amewapongeza washindi wa mbio hizo na kuwashukuru wadau, wasanii na washiriki wa mbio hizo, ambapo mwaka 2025 kumekuwa na jumla ya washiriki 2,000 kutoka washiriki 307 mwaka 2017.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema mbio hizo ni za kipee nchi nzima kwa vile wakimbiaji wanashiriki kwa siku mbili ili kutoa fursa kwao kushiriki kikamilifu.
Amesema awali mbio hizo zililenga kusaidia sekta ya elimu na afya pekee hata hivyo Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga shule na hospitali kwa wingi.
“ Kwa upande wa miundombinu hiyo, Serikali ya Dkt. Samia imefanya kazi kubwa na zile fedha tulizokuwa tunapeleka katika sekta ya afya sasa tunawakatia wananchi bima za afya, tayari tumekata bima za afya 9,000,” amesema Dkt. Tulia.
Ameendelea kusema kuwa katika sekta ya elimu wamewapatia madaftari na vifaa vya shule watoto zaidi ya 3,000 kupitia michango ya washiriki wa wadau wa mbio hizo. Aidha, wamejenga nyumba tatu na zipo tayari kwa ajili ya kugawa kwa watu wenye uhitaji.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amegawa zawadi kwa washindi wa msimu wa tisa wa mbio za Tulia.
MWISHO
0 Comments