NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
Wakati Tanzania inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais Mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitia Wilaya ya Iringa Mjini Islam Huwel ameonyesha imani kubwa kwa ushindi wa kishindo wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa anayewakilisha Wilaya ya Iringa Mjini, Islam Huwel, amesema kuwa hali ya kisiasa katika jimbo hilo ni ya utulivu na matumaini makubwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.
Akizungumza na Matukio Daima Media, Huwel alisema kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo umeongeza kujiamini kwa wana CCM wa Iringa Mjini, kwani mafanikio hayo yanajionyesha wazi na kugusa maisha ya wananchi wa kawaida.
Alisema hata vyama vya upinzani wamekuwa wakikiri mafanikio ya Serikali kutokana na jinsi ambavyo miradi ya maendeleo inawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.
“Leo hii Iringa Mjini kuna utulivu wa kisiasa, hata wapinzani hawana chokochoko kwa sababu wanashuhudia maendeleo makubwa yaliyotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Wananchi wananufaika, shule zimejengwa, barabara za lami zipo, vituo vya afya na hospitali zimeimarishwa, na miradi ya maji imekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wengi,” alisema Huwel.
Aliongeza kuwa kazi iliyofanywa na Rais Samia haiwezi kuelezeka kwa maneno machache, kwani ni kazi ya kiwango cha juu inayostahili kuungwa mkono na wananchi wote.
Alisema ni jukumu la kila mkazi wa Iringa kutambua na kuthamini kazi hiyo, na wakati ukifika, tathmini hiyo ionyeshwe kupitia kura kwa kumpigia Rais Samia pamoja na wagombea wa CCM katika ngazi ya ubunge na udiwani.
“Mafanikio haya makubwa hayawezi kutokea bila dhamira ya kweli ya kiongozi. Rais wetu ameonyesha dhamira hiyo, na sisi kama wana CCM hatuna budi kujivunia uongozi wake tunamshukuru kwa moyo wake wa huruma, ujasiri na uzalendo,” alisema Huwel.
Katika upande wa huduma za kijamii, Huwel alibainisha kuwa miradi ya maji imesaidia kwa kiwango kikubwa kumtua mama ndoo kichwani, jambo ambalo lilikuwa kero kubwa kwa muda mrefu.
Alisema kuwa maeneo mengi ya Wilaya ya Iringa Mjini sasa yanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika, hali inayoboresha afya, ustawi na maisha ya wananchi.
“Leo hii mama anajishughulisha na kazi nyingine za maendeleo kwa sababu maji yapo jirani. Zamani wanawake walikuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji, lakini sasa hayo ni historia. Serikali ya Awamu ya Sita imejitoa kwa vitendo,” alisema.
Pia alieleza kuwa sekta ya elimu imeimarika kwa kiasi kikubwa, huku shule mpya zikijengwa na za zamani zikikarabatiwa ili kutoa mazingira bora ya kujifunzia.
Alisema kuwa matokeo ya juhudi hizi yanaonekana kupitia ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi, na motisha kwa walimu kuendelea kutoa elimu bora.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali ya Rais Samia imewekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu. Hii ni hazina kwa taifa. Vijana wetu wanaweza kupata elimu bora karibu na makazi yao bila usumbufu, na hii inaongeza usawa na fursa kwa wote,” alisema.
Huwel alisema kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya wananchi na viongozi wa serikali, hasa kwenye kusimamia na kutunza miundombinu inayotekelezwa.
Alisema maendeleo ni matokeo ya ushirikiano na mshikamano baina ya viongozi na wananchi, na kwamba kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mafanikio hayo.
Katika sekta ya afya, alisema kuwa vituo vya afya na hospitali zimeongezeka na kuimarishwa, huku huduma za mama na mtoto zikipatiwa kipaumbele. Alieleza kuwa mafanikio haya yanatokana na maelekezo na maono ya Rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.
“Leo hii kuna dawa, kuna vifaa tiba, na huduma zinazotolewa katika vituo vyetu ni bora. Hii ni tofauti na zamani ambapo wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya,” alisema Huwel.
Alitoa wito kwa wananchi wa Iringa Mjini kutokubali kuyumbishwa na propaganda za kisiasa kutoka kwa wapinzani, akisisitiza kuwa ushahidi wa maendeleo upo wazi.
Alisema kuwa wakati wa uchaguzi ni fursa ya kuthibitisha imani kwa viongozi walioleta maendeleo, na si wakati wa kujaribu viongozi wasiokuwa na dira.
“Tuna kazi kubwa mbele yetu, na kazi hiyo ni kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kushika hatamu za uongozi ili kazi iendelee. Tunapaswa kuwa mabalozi wa maendeleo haya na kuwaeleza wengine ukweli wa kazi iliyofanyika,” alisema.
Hata hivyo alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na viongozi wa chama wilaya ya Iringa mijini chini ya mwenyekiti Said Rubeya na katibu wake kuwa wamekuwa na ushirikiano mkubwa pamoja na jumuiya zote za chama huku akimpongeza mwenezi wa CCM Iringa mjini Edo Bashir kwa kutangaza vema chama.
kwa ngazi ya mkoa wa Iringa alisema Mwwnyekiti CCM mkoa Daud Yassin na viongozi wengine wamekuwa hawalali kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya chama na kumpongeza Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Salim Abri Asas kuwa amekuwa nguzo ya maendeleo na uhai wa chama mkoa wa Iringa pamoja na viongozi wa serikali ya wilaya na mkoa . it
Islam Huwel alisema kuwa ushindi wa Rais Samia na CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa hautakuwa wa kawaida, bali utakuwa wa kishindo kutokana na rekodi ya utekelezaji bora wa Ilani ya CCM.
Hivyo alitoa wito kwa wana CCM Iringa Mjini kuendelea kuwa wamoja, waaminifu kwa chama chao na kuwa mstari wa mbele kuhamasisha upigaji kura kwa wagombea wa CCM ili kuhakikisha kuwa kazi ya maendeleo inaendelea kwa kasi zaidi.
0 Comments