Header Ads Widget

BENKI YA NMB YANYAKUA TUZO KIBAO KWA KUJALI USALAMA NA AFYA KWA WAFANYAKAZI WAKE




Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 


BENKI ya NMB imetunukiwa tuzo tano kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kutokana na hatua zinazochukuliwa na benki katika kuhakikisha mazingira salama na yenye afya kwa wafanyakazi na wateja wake.


Tuzo hizo zilitolewa juzi katika hafla ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete  kwenye maadhimisho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kwa mwaka 2025 yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida.


Katika hafla hiyo NMB ilitambuliwa kama kampuni nmbora kwenye sekta ya fedha na bima kwa kupata tuzo ya kwanza, na pia kutwaa tuzo ya pili kupitia Kanda ya Kati. Benki hiyo ilipata pia Tuzo ya Tatu kama Mshiriki Bora wa Maonesho ya OSHA.


Tuzo nyingine ya tatu NMB ilitambuliwa kuwa kampuni iliyoibeba vizuri kaulimbiu ya mwaka na pia ilipokea tuzo maalum ya kutambuliwa kwa mchango wake katika kufanikisha maonesho ya OSHA 2025.


Kikwete akizungumza katika hafla hiyo aliipongeza NMB pamoja na taasisi na makampuni mengine yaliyoshiriki na kwamba serikali itaendelea kuthamini na kuboresha mfumo wa utoaji tuzo za OSHA ili kuhamasisha uboreshaji wa usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.


Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango katika mahojiano na waandishi wa habari alisema imekuwa ikichukua hatua za kulinda usalama na afya za wafanyakazi na wateja wake ambapo kipo kitengo maalum cha kushughulikia masuala hayo kwa lengo la kuhakikisha ufanisi kazini unakuwepo.


Alisemasuala la kulinda usalama na afya kwa wafanyakazi  na wateja limekuwa ni jambo linalopewa kipaumbele cha kwanza katika benki hiyo.


"Elimu imekuwa ikitolewa kwa wafanyakazi wetu na vipo vifaa maalum kwenye matawi ya benki yetu ambavyo ikitokea janga lolote mfano la moto wanashughulika nalo lakini pia wapo wafanyakazi waliopewa mafunzo ya namna ya kukabiliana na majanga," alisema.


Shango alisema NMB imekuwa ikishirikiana na idara za serikali zinazojihusisha na masuala ya kukabiliana na majanga ili kunapotokea tatizo lolote wafanyakazi na wateja waweze kuokolewa.


Aidha,Shango alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuitumia Benki NMB kwani imekuwa ni salama na kurahisisha masuluhisho ya kiteknolojia katika utoaji wa huduma zake.


MWISHO.











Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI