wakili Laetitia Petro
Na Matukio Daima Media,Iringa
Kufuatia tukio la udhalilishaji watoto wa kike lililofanywa hivi karibuni kupitia Moja kati ya Vyuo vikuu nchini Tanzania Jukwaa la Women Inspire Women (WIW) imetoa Tamko la kulaani Matukio ya udhalilishaji watoto wa kike nchini .
Akizungumza na wanahabari Leo mwenyekiti wa Taasisi hiyo wakili Laetitia Petro Ntagazwa alisema wamepokea kwa masikitiko Makubwa taarifa ya udhalilishaji huo .
,"Sisi kama Women Inspire Women, tunalaani vikali tukio la udhalilishaji lililofanywa na kundi la wanafunzi wa kike dhidi ya mwanafunzi mwenzao wa kike, kama lilivyoonekana katika picha ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii"
,kuwa tukio hili ni kinyume na maadili ya utu, heshima ya binadamu, na halilingani kabisa na matarajio ya jamii kutoka kwa wasomi wa ngazi ya elimu ya juu.
"Ni ishara ya wazi ya ukosefu wa maadili, nidhamu na uelewa wa haki za binadamu miongoni mwa baadhi ya vijana wetu walioko vyuoni "
Alisema tukio hili linakiuka Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na sheria mbalimbali za nchi yetu.
"Tunapongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, kwa kuhakikisha kuwa manusura wa tukio hili anapatiwa msaada wa kisaikolojia, kisheria na kijamii "
Pia tunaunga mkono wito wa kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria wote waliokiuka sheria na taratibu husika.
Alisema pamoja na hatua hizo Bado wanalaani pia tukio jingine lililotokea tarehe 21 Machi 2025 katika eneo la Bagdadi, Mafinga – Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, ambapo wanawake wanne walimshambulia na kumjeruhi vibaya mwanamke mwenzao kwa tuhuma za kutoa siri za mapenzi.
"Ingawa tukio hilo liliripotiwa Polisi, hadi sasa hatua madhubuti hazijachukuliwa. Tunaitaka Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama kuhakikisha haki inatendeka".
Alisema Udhalilishaji na ukatili wa aina yoyote ni kosa la jinai na haupaswi kuvumiliwa kwa namna yoyote ile kuwa Elimu ya juu haipaswi kuwa uwanja wa kudhalilishana, bali ni jukwaa la kukuza fikra, utu na mshikamano wa kijamii.
Pia alisema ni wajibu wa kila mmoja wetu, kama sehemu ya jamii, kuwafundisha vijana wetu kuheshimu tofauti na kutatua migogoro kwa njia ya kistaarabu na kisheria.
Wakili huyo alisema Wanawake wanapaswa kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria katika kutatua changamoto mbalimbali.
Hata hivyo alitoa wito kwa Vyuo vikuu kuimarisha Madawati ya Jinsia na kutoa elimu endelevu kuhusu ukatili wa kijinsia na haki za binadamu,Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika malezi yenye maadili ya watoto na vijana na Wanafunzi kuzingatia maadili ya kitaaluma, utu wa binadamu, na kuheshimu sheria za nchi.
Pia Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka na za haki kwa kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha wahusika wote wanawajibishwa kisheria,Wananchi, wakiwemo wanawake, kutokujichukulia sheria mkononi pindi wanapokutana na changamoto, bali wafuate mifumo ya kisheria iliyowekwa.
Alisema kuwa Women Inspire Women (WIW) itaendelea kufuatilia kwa karibu matukio haya, na kusimama mstari wa mbele katika kulinda haki, kuhimiza uwajibikaji na kujenga jamii yenye usawa, utu na heshima kwa wote.
Kuwa Wiw ni jukwaa huru lililoanzishwa tarehe 28 Machi 2025, likiwa na lengo la kuwakutanisha wanawake wanasheria na mawakili kwa ajili ya kusaidiana, kushirikiana na kupeana msaada katika masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake na watoto nchini Tanzania.
0 Comments