Watu walionekana kukumbatiana na kulia katika eneo la shambulio huko Sumy
Shambulio la kombora la Urusi katika mji wa Sumy wa Ukraine, ambalo liliua watu 34 - ikiwa ni pamoja na watoto wawili - na kujeruhi wengine 117, limelaaniwa vikali na washirika wa Magharibi wa Kyiv.
Makombora mawili ya balistiki yalipiga katikati mwa mji Jumapili asubuhi, na kulipuka karibu na chuo kikuu cha serikali na kituo cha Congress, na kuacha miili iliyojaa damu kutawanyika mitaani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amelitaja shambulizi hilo kuwa "la kuogofya" huku kansela mtarajiwa wa Ujerumani, Friedrich Merz, akiishutumu Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita.
Hakukuwa na maoni rasmi ya mara moja kuhusu shambulio hilo kutoka Urusi, ambayo vikosi vyake katika mpaka wa karibu vinasemekana kujiandaa kwa mashambulizi makubwa.
Shambulio hilo limetokea wakati Marekani, mshirika mkubwa zaidi wa kijeshi wa Ukraine, imekuwa ikitafuta suluhu ya vita - sasa katika mwaka wake wa nne - kupitia mazungumzo chini ya Rais Donald Trump.
Kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemtaka Trump mwenyewe kutembelea Ukraine na kuona uharibifu uliosababishwa na shambulio la Urusi.
"Tafadhali, kabla ya aina yoyote ya maamuzi, aina yoyote ya mazungumzo, njoo uone watu, raia, wanajeshi, hospitali, makanisa, watoto walioharibiwa au waliokufa," alisema Jumapili katika mahojiano ya kipindi cha Dakika 60 cha CBS.
Akitoa salamu zake za rambirambi kwa wapendwa wa waathiriwa, Rubio, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, alisema shambulio hilo ni "kumbukumbu ya kusikitisha" kwa nini utawala wa Trump "unaweka muda mwingi na juhudi kujaribu kumaliza vita hivi".
Hapo awali, mjumbe maalum wa Trump nchini Ukraine, Luteni Jenerali mstaafu Keith Kellogg, alitumia lugha kali zaidi, akisema shambulio hilo limevuka "mstari wowote wa adabu". Merz, ambaye anatarajiwa kuchukua wadhifa wa kansela mpya wa Ujerumani mwezi ujao, aliliambia shirika la utangazaji la Ujerumani ARD kwamba shambulio dhidi ya Sumy lilijumuisha "uhalifu mkubwa wa kivita".
"Kilikuwa kitendo cha kihuni.. na ni uhalifu mkubwa wa kivita, wa makusudi na uliokusudiwa," mwanasiasa huyo wa kihafidhina alisema.
0 Comments