Na Matukio Daima App.
Vijana 110 wa umri wa kati ya Miaka 17 Hadi 25 waliowahi kuishi na kufanya kazi mitaani wanaohudumiwa na Mtandao wa Safina street network wenye Makao yake makuu mjini Morogoro wamejitokeza kuchangia damu kwa hiyari Ili kusaidia kuokoa maisha ya wahitaji wakiwemo kina mama wajawazito, watoto wachanga na majeruhi.
Vijana hao ambao wengi wao kwa sasa wanaendelezwa katika vyuo vya kati, vyuo vikuu na wengine wameshahitimu kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakishiriki kuchangia Damu kwa mwaka wa nne mfululizo pindi wanapokutana kwa Kambi maalum katika Makao makuu ya Safina street network kata ya Mzinga manispaa ya Morogoro.
Baadhi ya vijana waliokutwa wakichangia Damu kambini hapo, Abasi Mwinuka, Joseph Matreka na Selemani Nazareth kwa nyakati tofauti walisema wanaguswa kujitolea Damu kutokana na kutambua mahitaji makubwa ya Damu yaliyopo huku Baadhi ya watu wakipoteza maisha kwa kukosa damu.
Walibainisha licha ya mwaka wa nne sasa kuwa wanachangia Damu hawajawahi kupata madhara yeyote kiafya na wanaona kitendo hicho ni thawabu kiimani na faraja kumuokoa mhitaji ikizingatiwa kuwa Damu haiuzwi hivyo ni lazima watu wajitokeze kuchangia.
Naye Mkurugenzi wa Huduma kutoka Safina Street network, Nicolaus Duma alisema wanahudumia watoto na vijana zaidi ya 300 kituoni hapo ambapo wengine hawakuweza kuchangia kutokana na umri wao kuwa mdogo na kwamba zoezi hilo wamekuwa wakishiriki kwa hiyari bila kushurutishwa.
Akasema vijana hao wamekuwa wakiwapata kutoka mitaani wakiwemo watoto wadogo na kwamba Kazi hiyo wamekuwa wakiifanya bila faida yeyote Ili kuonesha upendo kwao baada ya kukutana na madhila mbalimbali ikiwemo kubaguliwa na kukatiliwa na jamii.
Akatolea mfano mwaka jana walipata shida kwa kijana mmoja kuwa na uhitaji wa Damu, lakini walipiga simu hospitali ya Mkoa na kijana huyo kusaidika mara moja hadi kupelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi hivyo ni umuhimu kuchangia damu wakati wote ili kuwanusuru wahitaji.
"Pamoja na jitihada hizi, tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kutoa huduma zinazokidhi viwango hapa makao makuu ikiwemo ya ubovu wa barabara, ukosefu wa Umeme wa TANESCO unaotullazimu kutumia Umeme wa jua hivyo kushindwa kufunga Miundo mbinu ya kuwawezesha vijana hawa stadi mbalimbali za ufundi"Alisema Duma.
Akataja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa maji unaowalazimu vijana kutafuta umbali mrefu hivyo kuomba Serikali hususani kupitia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwaangalia kwa jicho la kipekee kama Mama na kama mlezi Ili wafikishiwe huduma hizo ikiwemo Umeme wa REA kwani gharama kufikisha Umeme na maji kutoka ulipopita mtandao ni gharama kubwa ambazo hawawezi kumudu.
Kiongozi huyo akapongeza ushirikiano walio nao na Mamlaka mbalimbali za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi, idara ya maendeleo ya Jamii na ustawi wa jamii na wadau wengine kuhakikisha ustawi wa watoto na vijana hao unafikiwa.
Kwa upande wake mratibu wa Damu salama kutoka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt Ileme Wilson, akiongoza zoezi hllo, Alisema kwa sasa hospitali hiyo Peke yake inatumia karibu uniti 15 Hadi 20 kila siku kwaajili ya kusaidia wahitaji watoto wachanga,kina mama wajawazito, wanafanyiwa operesheni, wenye selimundu, majeruhi nk na mahitaji ya Damu bado ni makubwa.
Akawashukuru vijana hao wa Safina street network kwa msaada huo kwa mwaka wa nne mfululizo huku akiisihi jamii kujitokeza kuchangia damu kwani haiuzwi na inapatikana kwa watu huli mahitaji yakiendelea kuwa makubwa siku Hadi siku.
Mratibu huyo wa Damu Salama akawaondoa hofu wananchi kuwa kuchangia damu hakuna madhara yeyote kiafya kama kudhoofu ama kutoa mwanya kwa mlipuko wa magonjwa badala yake kufanya hivyo husaidia kuimarisha kinga za mwili na na kufanya seli za mwili kuwa imara zaidi.
Mwisho
0 Comments