Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Urusi na Ukraine "ziko karibu kabisa kufikia makubaliano", saa chache baada ya mjumbe wake maalum, Steve Witkoff, kufanya mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, mjini Moscow.
Trump, ambaye alizungumza na waandishi wa habari alipowasili nchini Italia kwa ajili ya mazishi ya Papa Francis, alisema ilikuwa “siku nzuri” ya mazungumzo ya amani.
Wakati huo huo, Kremlin ilielezea mazungumzo hayo ambayo Ukraine haikuhudhuria kuwa "ya kujenga". Kupitia mitandao ya kijamii, Trump alidai kuwa “sehemu kubwa ya masuala muhimu yamekubalika” na akazitaka pande zote mbili kukutana “katika ngazi za juu” ili “kukamilisha makubaliano hayo”.
Hata hivyo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, katika hotuba yake ya video iliyotolewa Ijumaa jioni, alisema kuwa “shinikizo la kweli kwa Urusi linahitajika” ili kukubali usitishaji mapigano usio na masharti.
Mapema siku hiyo, aliliambia Shirika la Habari la BBC kuwa masuala ya mipaka kati ya Kyiv na Moscow yanaweza kujadiliwa ikiwa kutakuwa na “usitishaji kamili na usio na masharti wa mapigano”.
Ripoti zinaeleza kuwa chini ya mapendekezo ya amani ya Marekani, Ukraine huenda ikalazimika kukubali kupoteza maeneo makubwa ambayo tayari yamevamiwa na kuunganishwa na Urusi. Trump pia amesema kuwa anaunga mkono Urusi kuendelea kuimiliki eneo la Crimea, ambalo lilichukuliwa kinyume cha sheria na Moscow mwaka 2014 jambo ambalo Rais Zelensky amekataa katakata.
Urusi ilianzisha uvamizi mkubwa dhidi ya Ukraine mwaka 2022 na kwa sasa inadhibiti takribani asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine.
0 Comments