Header Ads Widget

TUDUMISHE MUUNGANO KWA KUUNGA MKONO KAZI ZA RAIS DKT SAMIA NA DKT MWINYI -WAKILI MBEDULE

 



Na Matukio Daima Media 

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 61 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, Muungano ulioasisiwa tarehe 26 Aprili 1964 na kuwa chimbuko la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Katika maadhimisho haya ya kihistoria, Wakili Sosten Mbedule ametoa rai kwa wananchi wote kutafakari kwa kina thamani ya Muungano huu na kushiriki kikamilifu katika kuuendeleza.

Akizungumza kuhusu maadhimisho haya, Wakili Mbedule alisema, “Muungano wetu ni tunu yetu. Ni msingi wa amani, mshikamano na maendeleo tuliyonayo.


 Tudumishe Muungano huu kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.”

Ameeleza kuwa viongozi hao wawili wameonesha kwa vitendo dhamira ya kulinda na kuimarisha Muungano kwa kuhakikisha kuwa Watanzania wote kutoka pande mbili za Muungano wananufaika kwa usawa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

 Ametoa mfano wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile miundombinu ya barabara, nishati, afya na elimu ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi, tumeona namna ambavyo Muungano umeendelea kuwa nguzo ya mafanikio ya taifa letu. 

Ni jukumu letu kama wananchi kuunga mkono juhudi hizi na kuhakikisha tunadumisha Muungano huu kwa mshikamano, heshima na moyo wa uzalendo,” alisema Mbedule.

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Muungano Wetu ni DHAMANA, Heshima na Tunu ya Taifa”, inalenga kuwahimiza Watanzania kutambua kuwa Muungano huu si wa viongozi pekee, bali ni wa wananchi wote na hivyo kila mmoja anayo nafasi ya kuuenzi na kuutetea.



Aidha, Wakili Mbedule amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 kama njia ya kuimarisha demokrasia na kulinda misingi ya Muungano. 

Ameeleza kuwa sauti ya kila raia ni muhimu katika kuhakikisha taifa linapata viongozi bora watakaodumisha Muungano na kusimamia haki, usawa na maendeleo kwa wote.

“Kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kizalendo. Ni namna ya kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa taifa na katika kuulinda Muungano wetu,” alisema.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kutanguliza umoja, mshikamano na uzalendo, akisisitiza kuwa bila Muungano, taifa hili lisingekuwa na nguvu na heshima kubwa iliyo nayo leo ndani na nje ya mipaka yake.

Kheri ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania – Tudumishe kwa Vitendo!



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI