Donald Trump amemlaumu Volodymyr Zelensky kwa kuanzisha vita na Urusi siku moja baada ya shambulizi kubwa la Urusi kuwaua zaidi ya watu 30 nchini Ukraine.
Rais wa Marekani alisema kiongozi huyo wa Ukraine alizungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin juu ya "mamilioni ya watu waliokufa" katika vita vya Ukraine.
"Huwezi kuanzisha vita dhidi ya mtu ambaye ni mara 20 ya ukubwa wako na kisha kutumaini kwamba watu watakupa makombora fulani," aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, ambapo pia alimlaumu Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden kwa mzozo huo.
Matamshi ya Trump yanajitokeza baada ya ghadhabu iliyoenea juu ya shambulio la Urusi kwenye mji wa Sumy wa Ukraine siku ya Jumapili, ambalo lilikuwa shambulio baya zaidi la Urusi dhidi ya raia mwaka huu.
Trump alisema hapo awali shambulio la Urusi lilikuwa "kosa".
"Mamilioni ya watu walikufa kwa sababu ya watu watatu," Trump alisema Jumatatu. "Wacha tuseme Putin nambari moja, tuseme Biden ambaye hakujua ni nini alichokifanya, nambari mbili, na Zelensky."
Inakadiriwa kuwa mamia ya maelfu, lakini sio "mamilioni", ya watu wameuawa au kujeruhiwa kila upande tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili wa Ukraine mnamo 24 Februari 2022.
Akihoji uwezo wa Zelensky, Trump alisema kuwa kiongozi huyo wa Ukraine "siku zote alikuwa akitafuta kununua makombora".
"Unapoanzisha vita, lazima ujue unaweza kushinda," rais wa Marekani alisema.
Mvutano kati ya Trump na kiongozi huyo wa Ukraine umekuwa mkubwa tangu makabiliano yao makali katika Ikulu ya White House mwezi Februari.
Katika mahojiano kabla ya shambulizi la hivi punde zaidi la Urusi, Zelensky alimtaka Trump kutembelea Ukraine kabla ya kufanya makubaliano na Putin kumaliza vita.
Mashambulizi ya Urusi katika mji wa Sumy yaliua takriban watu 35 na kujeruhi wengine 117 .
Moscow ilisema kuwa ilirusha makombora mawili ya Iskander katika mkutano wa wanajeshi wa Ukraine, na kuua 60 kati yao, lakini haikutoa ushahidi wowote.
Trump alisisitiza kuwa anataka "kukomesha mauaji" na kuashiria kutakuwa na mapendekezo hivi karibuni, lakini hakufafanua.
0 Comments