Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Seki Boniventure Kasuga, ameendelea kuonesha moyo wa uzalendo na uwajibikaji kwa jamii kwa kutoa mchango wa fedha taslimu Shilingi 600,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya waasisi wa Shule ya Sekondari ya Wazazi Ukumbi, pamoja na kusaidia ukarabati wa vyoo vya wavulana katika shule hiyo iliyopo Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa.
Mchango huo alitoa wakati wa mahafali ya kidato cha sita yaliyofanyika Aprili 29, ambapo Kasuga alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kasuga alisema kuwa mchango wake ni sehemu ya kuitikia wito wa jamii na shule hiyo ambayo inamilikiwa na jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa.
Akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, Kasuga alitembelea miundombinu ya shule hiyo na kujionea changamoto zilizopo, ikiwemo hali duni ya vyoo vya wavulana na mahitaji ya heshima kwa waasisi wa shule kwa kujengewa nyumba maalumu ya kumbukumbu.
Alisema kwamba hatua hiyo ni muhimu si tu kwa kuboresha mazingira ya elimu, bali pia kwa kuheshimu historia na mchango wa walioweka msingi wa taasisi hiyo.
Katika hotuba yake, aliwapongeza wahitimu wa kidato cha sita kwa hatua muhimu waliyofikia katika safari yao ya elimu. Alisisitiza kuwa mafanikio yao ni matokeo ya juhudi zao binafsi, ushirikiano wa walimu na wazazi, pamoja na mazingira wezeshi yaliyoandaliwa na serikali.
“Napenda niwapongeze sana kwa kufika hapa mlipo hi hatua muhimu, lakini pia ni mwanzo wa safari mpya yenye changamoto, majukumu, na fursa nyingi Mjitahidi kutunza heshima mliyopata kwa njia ya kujituma zaidi, kuwa na nidhamu, na kuendelea kujifunza kwa bidii,” alisema Kasuga.
Kasuga alisema kuwa serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari nchini, lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo wazazi na kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu.
Alitoa rai kwa wazazi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora kwa kuwapeleka shule na kushiriki maendeleo ya taasisi za elimu.
Aidha, aliwapongeza walimu na watumishi wote wa shule ya Ukumbi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kufundisha na kulea vijana kwa weledi, moyo wa kujitolea, na uzalendo.
Alisema kuwa mafanikio ya wanafunzi hawawezi kutokea bila uwepo wa walimu wenye maono, moyo wa kujenga, na nidhamu ya kazi.
Katika hatua nyingine, Kasuga alitumia jukwaa hilo kutoa wito mahsusi kwa wahitimu na vijana kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato wa demokrasia, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Alisema kuwa sauti ya vijana ni silaha kubwa ya mabadiliko chanya katika taifa, hivyo wasisite kujitokeza kujiandikisha na kupiga kura kwa uamuzi wa busara.
“Kura yako si haki tu, bali ni chombo chenye nguvu cha kushiriki maamuzi ya taifa na kusaidia kuleta maendeleo Vijana ndiyo nguzo ya taifa.
Ushiriki wenu kwenye uchaguzi ni muhimu kwa kuhakikisha mabadiliko yanayolenga maslahi ya wengi yanafikiwa,” alisisitiza.
Pia aliwahimiza vijana kuiona elimu kama daraja la kuwavusha kuelekea maisha yaliyojaa fursa, changamoto na wajibu.
Alieleza kuwa elimu ya kweli haipo tu katika vitabu, bali katika kujijenga kimaadili, kiakili na kijamii.
“Elimu si tu kuhusu kusoma vitabu; ni kuhusu kuwa na udadisi, ujasiri, bidii na tabia njema Dunia ya sasa inahitaji viongozi wabunifu, wastahimilivu, wenye maono na walio tayari kutoa mchango wao kwa jamii. Kamwe msipoteze imani ndani yenu. Leo ni mwisho wa hatua moja, lakini ni mwanzo wa njia nyingine mpya yenye nafasi nyingi," alisema.
Akimzungumzia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kasuga alisema kuwa uongozi wake umekuwa mfano wa kuigwa katika Afrika kutokana na maono ya maendeleo na utekelezaji wa miradi mikubwa kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), miradi ya kimkakati ya nishati, afya, elimu, pamoja na uwekezaji wa kisasa kwenye bandari ya Bagamoyo.
Alisema mafanikio haya ni fursa kwa vijana kujifunza kuwa kila ndoto inaweza kufikiwa kwa bidii na kujituma.

Walisema kuwa jitihada za kuimarisha miundombinu ya shule zinaendelea na mchango huo utasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi inayoendelea.
“Tunaendelea kuhamasisha wadau wengine wa maendeleo, wazazi, na jamii kwa ujumla kuiga mfano huu wa Mjumbe wetu wa Kamati ya Siasa.
Tunaamini kuwa kwa mshikamano, kila changamoto ya shule hii inaweza kutatuliwa,” alisema mmoja wa viongozi wa shule hiyo.
Shughuli za ujenzi wa nyumba ya waasisi pamoja na ukarabati wa vyoo vya wavulana zimekwishaanza na zinaendelea kwa kasi, zikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi, pamoja na kuhifadhi historia ya shule hiyo ambayo imekuwa chimbuko la viongozi wengi katika wilaya ya Kilolo na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Katika hitimisho lake, Kasuga aliwataka wahitimu kutambua nafasi yao katika jamii na kuwa mabalozi wa mabadiliko popote watakapokuwa.
Alisema kuwa taifa linawategemea vijana wenye fikra chanya, wenye dira, na waliojengwa katika misingi ya uzalendo, kujituma na uwajibikaji.
0 Comments