Header Ads Widget

MRADI WA REST WAANZA KUWAWEZESHA WENYE ULEMAVU MKOANI IRINGA KUSHIRIKI KATIKA MAENDELEO NA UCHUMI


Na Matukio Daima Media,Iringa 

Mradi wa Reproductive Equity Strategic Tanzania (REST) umeanzisha rasmi kampeni maalum ya kutoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu mkoani Iringa, ukiwa na lengo la kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na  kiuchumi 


Kupitia mafunzo hayo, Mradi wa REST unalenga kuondoa vikwazo vya kimfumo na kijamii vinavyowakabili watu wenye ulemavu, pamoja na kuhakikisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinatambua na kuzingatia ushirikishwaji wa kundi hilo katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa REST, Celina Protas, alisema kuwa moja ya changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu ni kutengwa na kutopewa nafasi sawa ya kushiriki katika michakato muhimu ya kijamii kama vile uchaguzi, ajira, elimu na huduma nyingine za kijamii.


"Hatutafikia maendeleo ya kweli kama taifa hadi pale kila mtu atakapopata nafasi sawa ya kushiriki katika michakato ya maendeleo bila kujali hali yake ya kimwili au kiakili. Watu wenye ulemavu wanapaswa kupewa heshima yao na kushirikishwa katika kila hatua ya ujenzi wa taifa," alisema Celina.


Aliongeza kuwa mradi huo umejikita pia katika kuwaelimisha viongozi wa serikali, mashirika ya kiraia na wanajamii kwa ujumla ili kubadili mitazamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu, na badala yake kuwaona kama rasilimali muhimu katika jamii.


Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa,  Fatuma Mohamed  alisema kuwa jamii nyingi bado zimekuwa na mitazamo ya kuwabagua watu wenye ulemavu, hali inayosababisha kundi hilo kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo.


"Watu wenye ulemavu wana haki sawa kama watu wengine. 


Kuwa hili ni jambo ambalo kila mmoja wetu anapaswa kulielewa. Ni wajibu wetu kama viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha tunawawezesha watu hawa kupata fursa sawa," alisema  Fatuma.


Alisisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaendelea kutoa ushirikiano kwa miradi kama REST ambayo inalenga kuondoa ubaguzi na kuweka misingi ya usawa kwa kila mwananchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Iringa,  Shabani Shomari, alipongeza mradi huo kwa kuona umuhimu wa kundi hilo katika maendeleo ya taifa.


"Kwa muda mrefu tumekuwa tukihangaika kutambuliwa kama sehemu ya jamii yenye mchango katika maendeleo, lakini mara nyingi tumesahaulika. Kupitia mradi huu, tunahisi tumetambuliwa na tunapata nafasi ya kujiamini zaidi," alisema  Shabani.


Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanasaidia kuwatia moyo watu wenye ulemavu kujitokeza kushiriki katika siasa na nafasi za uongozi, jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likionekana gumu kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo vikwazo vya kimazingira, mitazamo ya kijamii, na ukosefu wa taarifa.


Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, asilimia kubwa ya watu wenye ulemavu nchini bado hawajafanikiwa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki, elimu sahihi juu ya haki zao, pamoja na mitazamo hasi kutoka kwa jamii.

Mradi wa REST unaendeshwa kwa ushirikiano wa karibu na Taasisi zisizo za kiseriksli pamoja nab serikali na wadau wa maendeleo, na umejipanga kufikia mikoa mbalimbali nchini kwa kutoa mafunzo na elimu ya haki za binadamu, ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, pamoja na kuwajengea uwezo wa kujitambua na kujieleza katika jamii.


Celina alisisitiza kuwa mradi huu hautabaki tu kwenye kutoa elimu bali pia utahamasisha utekelezaji wa sera na mikakati ya taifa inayohusu haki na usawa kwa watu wenye ulemavu.


Hata hivyo  Fatuma Mohamed  alitoa rai kwa jamii ya Iringa na taifa kwa ujumla kubadili mitazamo yao na kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu, bali kuwaona kama washiriki halali wa maendeleo.


"Tuache kuwa na huruma zisizo na tija, badala yake tuwape fursa ya kuthibitisha uwezo wao kwa vitendo. 


Tunaweza kuwa taifa lenye usawa na mshikamano wa kweli tukiwajumuisha wote," alihimiza.

Kwa sasa, mafunzo hayo yataendelea katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Iringa kwa kushirikisha watu wenye ulemavu kutoka makundi tofauti, ikiwemo wale wa uoni hafifu, usikivu, viungo, pamoja na ulemavu wa akili, kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuondoa hofu ya kushiriki katika michakato ya kijamii ikiwemo uchaguzi mkuu ujao.


Kwa upande wao washiriki wa mafunzo wameeleza kufurahishwa na jitihada hizo, wakisema kuwa ni mwanzo wa matumaini mapya kwa watu wenye ulemavu nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI