Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa Daud Yassin (Kushoto) akimkabidhi MNEC Salim Abri Asas tuzo
Na Matukio Daima Media
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Abri maarufu kama "Asas", ameendelea kuwa kielelezo cha uongozi wa mfano kupitia mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya jamii na uhai wa Chama ndani ya Mkoa wa Iringa. Kupitia moyo wake wa uzalendo, huruma na mapenzi ya dhati kwa wananchi, Salim Abri amekuwa mstari wa mbele si tu katika kuimarisha misingi ya CCM bali pia katika kuboresha huduma muhimu za kijamii kwa vitendo vinavyoleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa Iringa.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Salim Abri ameweka historia kwa kufanikisha ujenzi wa miradi mikubwa ya kijamii ambayo imekuwa nguzo muhimu kwa ustawi wa wananchi wa Iringa na maeneo ya jirani.
Miongoni mwa miradi hii ni ujenzi wa wodi ya watoto njiti, hatua ambayo imeokoa maisha ya watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda na kuongeza matumaini kwa wazazi waliokuwa wakikumbwa na changamoto hizo.
Wodi hiyo imejengwa kwa viwango vya kisasa na vifaa muhimu vinavyowezesha utoaji wa huduma bora za kitabibu kwa watoto wachanga wenye uhitaji maalum.
Aidha, Salim Abri amejitokeza kama nguzo ya afya mkoani Iringa kwa kusaidia ujenzi wa Kituo cha Damu Salama, mradi ambao ni wa kipekee kwa kuwa unahakikisha upatikanaji wa damu salama kwa wagonjwa mbalimbali katika hospitali na vituo vya afya.
Kupitia kituo hiki, maisha ya wengi yameokolewa, na upatikanaji wa damu umekuwa rahisi zaidi kwa wale wanaohitaji hasa katika hali za dharura.
Si hivyo tu, ASAS pia ameshiriki kwa kiwango kikubwa kujenga na kuboresha vituo vya afya, ambavyo vimeongeza kasi ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa. Uwepo wa vituo hivi umeondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu na hivyo kuimarisha afya za wananchi.
Pamoja na hayo, amefanikisha ujenzi wa Jengo la Ustawi wa Jamii, jengo linalotoa huduma kwa makundi maalum kama wazee, walemavu, na watoto walioko katika mazingira hatarishi. Hili ni jengo muhimu linalowahudumia wananchi kwa upendo na heshima, sambamba na misingi ya haki za binadamu ambayo CCM imekuwa ikiisimamia.
Mbali na miradi mikubwa, Salim Abri ASAS hajawasahau watu mmoja mmoja wanaokumbwa na matatizo mbalimbali. Amekuwa akitoa msaada wa moja kwa moja kwa mtu mmoja mmoja, ikiwemo kugharamia matibabu, elimu, malazi na mahitaji mengine ya msingi kwa wahitaji.
Hii ni ishara ya uongozi wenye maono na moyo wa huruma, jambo linalowafanya wananchi waendelee kumheshimu na kumkubali kama kiongozi wa mfano.
Ikumbukwe kuwa michango ya Salim Abri imeendelea kuiheshimisha CCM mkoani Iringa, na kuonesha kwa vitendo kuwa chama hiki kinajali maisha ya wananchi wake. Anaakisi maono ya Chama Tawala kuhusu maendeleo jumuishi na ya watu. Kupitia juhudi zake, CCM imezidi kupata heshima kubwa kwa wananchi ambao wanashuhudia matunda ya uongozi bora. Ni wazi kuwa Salim Abri ameweka alama isiyofutika katika historia ya Iringa na CCM kwa ujumla.
0 Comments