Marekani yasema mazungumzo na Iran kuhusu makubaliano mapya ya nyuklia yanaendelea vizuri. Akizungumza kabla ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika Oman siku ya Jumamosi, Rais Trump alisema uamuzi unaweza kufikiwa katika siku chache zijazo.
Rais huyo wa Marekani, ambaye alijiondoa katika makubaliano hayo yaliyohusisha mataifa 25, alitishia kuishambulia Iran iwapo makubaliano mapya hayatafikiwa. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Rais Trump alisema ana matumaini kuhusu mazungumzo hayo na Iran.
Rais wa Marekani Donald Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano ya awali ya nyuklia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani mwaka 2018, na kwa muda mrefu amesema atafanya makubaliano yenye "tija".
Iran ilikuwa imekataa kujadili tena makubaliano hayo. Mazungumzo hayo mapya yanaonekana kama hatua muhimu ya kwanza ya kubainisha iwapo makubaliano yanaweza kufanyika, huku mikutano ya Jumamosi ikitarajiwa kulenga kuweka msingi wa mazungumzo.
Ni kiwango cha juu zaidi cha mazungumzo tangu muhula wa kwanza wa Trump madarakani, lakini haijabainika iwapo pande hizo mbili zitaketi katika chumba kimoja. Rais Trump amesema tu kwamba Iran haiwezi kuwa na silaha ya nyuklia.
Iran inatarajia makubaliano ya kuweka kikomo, lakini sio kusambaratisha, mpango wake wa nyuklia ili kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo.
0 Comments