Header Ads Widget

MAZUNGUMZO YA KWANZA YA MOJA KWA MOJA KATI YA DRC NA WAASI WA M23 KUFANYIKA LEO HUKO DOHA


Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kundi la waasi la M23 wanatazamiwa kufanya mazungumzo yao ya kwanza ya moja kwa moja leo mjini Doha.

Hii inaashiria hatua iliyopigwa kuelekea juhudi za kumaliza moja ya migogoro mikali zaidi katika Afrika ya Kati katika miongo kadhaa.

DRC, Umoja wa Mataifa na majumuiya ya kikanda yanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23 na kuwapa msaada wa silaha na kijeshi, ingawa Kigali inakanusha hili.

Akihutubia wakati wa shughuli ya kuashiria mwanzo wa mfululizo wa kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 jana Jumanne, Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema bila kuzitaja nchi zozote, kuwa zinapaswa kuyashughulikia matatizo yao na kumuwacha yeye akabiliane na ya kwake.

Mwezi Desemba mwaka jana, mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Angola yalivunjika baada ya Rwanda kuitaka serikali ya Congo kuzungumza moja kwa moja na M23.

Siku moja baada ya M23 kujiondoa kwa mazungumzo ya amani ,tarehe 18 mwezi Machi Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame walikutana nchini Qatar kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana mpatanishi mkuu akiwa ni Amir wa Qatar.

Haya yanajiri baada ya Angola kujiondoa kama mpatanishi mkuu wa mzozo kati ya Kongo na M23.

Kundi la waasi lilisonga mbele kwa kasi, na kuchukua udhibiti wa miji miwili muhimu - Goma na Bukavu.

Mzozo wa mashariki mwa Kongo umedumu kwa muda sasa, madini yakitajwa kama kichochea kikubwa. Mzozo umeongezeka haraka tangu Januari 2025, na maelfu ya watu waliuawa na mamia ya maelfu kulazimishwa kuyakimbia makazi yao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI