Jeshi la Sudan limefanya mashambulizi makubwa magharibi mwa Omdurman, na kutwaa tena taasisi muhimu kutoka kwa Vikosi vya RSF.
Ilichukua tena kambi ya kijeshi ya Al-Nusur, kituo cha polisi, na sehemu kubwa za Dar al-Salam na Al-Quwa, na kukata njia za usambazaji za RSF.
Katika hatua tofauti, jeshi pia linadai kuwa limeuteka tena mji wa Al-Silik na kambi ya karibu katika jimbo la Blue Nile baada ya shambulio la kushtukiza, huku mapigano yakizidi katika pande nyingi.
Wakati huo huo, ndege zisizo na rubani za RSF zililipua Bwawa la Merowe mara mbili chanzo kikuu cha umeme cha Sudan na kusababisha kukatika kwa umeme.
Jeshi lilisema ulinzi wake wa anga ulizuia mashambulizi lakini wakaonya juu ya hujuma kwa miundombinu muhimu.
Mashambulizi kama hayo siku zilizopita pia yalisababisha kukatika kwa umeme.
Jeshi linaishutumu RSF kwa kutumia ndege zisizo na rubani zinazotolewa na falme za kiarabu UAE, madai ambayo yamekanwa na waasi hao huku mzozo huo ukiingia mwaka wake wa tatu.
Lakini ingawa SAF inaonekana kuwa na kasi kwa sasa, ni vigumu kwa upande wowote kushinda vita kwa namna itakayowaruhusu kutawala Sudan nzima, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya International Crisis Group. Hata hivyo, pande zote mbili zimedhamiria kuendelea kupigana kwa ajili ya maeneo yaliyosalia, na juhudi za kufufua mazungumzo ya amani hadi sasa zimeshindwa.
Umoja wa Mataifa umeelezea hali nchini Sudan kama janga baya zaidi la kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kukimbia makazi yao na mamilioni wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku sehemu za nchi zikielekea kwenye njaa.
0 Comments