NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Ikumbukwe kuwa Tanzania leo inaadhimisha miaka 61 tangu kuundwa kwa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar mnamo tarehe 26 Aprili 1964, hatua muhimu na ya kihistoria iliyoasisi taifa lenye mshikamano, amani na umoja barani Afrika.
Ifahamike kuwa Muungano huu umeendelea kuwa nguzo ya mafanikio ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa Watanzania wote, na umekuwa mfano bora wa kuigwa na mataifa mengine duniani.
Akizungumza katika kuadhimisha siku hii adhimu, mdau wa maendeleo wilayani Kilolo mkoani Iringa Aidan Mlawa amesema kuwa Muungano wa Tanzania ni dhamana kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuulinda, kuudumisha na kuuenzi.
Ameeleza kuwa Muungano huu si tu ni makubaliano ya kikatiba, bali ni kiapo cha kindugu kilichojengwa juu ya misingi ya upendo, usawa na mshikamano wa kweli.
“Tunaposherehekea miaka 61 ya Muungano, tujiulize pia tumeufanyia nini Muungano huu? Je, tunautendea haki kama tunavyopaswa? Muungano huu ni heshima yetu kama taifa, ni tunu ambayo haipaswi kupuuzwa wala kutumika kisiasa, bali tulinde msingi wake,” amesema Wakili Mbedule.
Ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 kwa amani, upendo na nidhamu, ili kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kupata viongozi bora watakaolinda maslahi ya Muungano na wananchi kwa ujumla.
Amesema ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ni ishara ya kuuenzi Muungano kwa vitendo na kuendeleza misingi ya demokrasia na utawala bora.
“Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni fursa kwa kila Mtanzania kutimiza wajibu wa kizalendo. Kupiga kura ni haki, lakini pia ni wajibu wa kulinda msingi wa taifa letu.
Hatuwezi kuzungumzia Muungano bila kuhusisha sauti ya wananchi katika uamuzi wa uongozi wa nchi yao,” ameongeza.
Katika kipindi cha miaka 61, Muungano wa Tanzania umewezesha mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za kijamii kama elimu, afya, miundombinu, pamoja na kukuza mahusiano ya kidiplomasia na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Haya yote ni matokeo ya mshikamano uliokita mizizi kupitia Muungano huu adhimu.
Kauli mbiu ya mwaka huu, “Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Muungano Wetu ni DHAMANA, Heshima na Tunu ya Taifa” inawakumbusha Watanzania kuwa Muungano ni zawadi ya pekee kutoka kwa waasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Ni wajibu wa kila raia kuuenzi, kuutetea na kuukuza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mlawa amehitimisha kwa kuwatakia Watanzania wote kheri ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano huku akisisitiza kuwa mshikamano wa kweli utaendelezwa kupitia mshiriki wa kila mmoja katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Mlawa amesema anapongeza uamuzi wa serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa sherehe za Muungano Zifanyike Kila mkoa na kuwa kwa upande wake kama Mdau maendeleo amefika mkoa wa Mbeya na Songwe kushiriki na wadau wengine wa maendeleo kujionea namna shughuri za ujenzi wa Mundo mbinu ukiendelea Kwa Kasi hasa ya viwanja vya Ndege kama Uwanja wa Songwe .
Kheri ya Miaka 61 ya Muungano – Tanzania Daima!
0 Comments