Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) inatumia Sh.Bilioni 9.2 kila mwaka kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni mkakati wa kuunga mkono serikali jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha, kampuni hiyo imewaalika wananchi wa ndani na nje ya Mkoa wa Singida kufika katika banda la GGML kwenye maonesho ya wiki ya usalama na afya yalitoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kujifunza teknolojia za kisasa za uchimbaji madini.
Afisa Msimamizi Ardhi ofisi ya Mahusiano, John Kibiti, akizungumza na waandishi wa habari leo amesema hayo kwenye maonesho ya wiki ya usalama na afya yalitoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ambayo yameanza Aprili 24 mwaka huu kwenye viwanja sabasaba Mandewa Manispaa ya Singida na yatahitimishwa Aprili 30.
Amesema GGM ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti,imekuwa ikipewa maelekezo na serikali fedha hizo zinazotengwa ziwe zinaelekezwa kutekeleza miradi katika sekta ya afya,elimu,mazingira,miundombinu, sanaa na michezo.
"Katika sekta ya elimu tumeweza kujenga shule na madarasa zaidi 1000,tumepeleka madawati kwenye shule mbalimbali zaidi ya 30,000,kwenye afya tumejenga vituo vya afya 50,majengo ya kupokea wagonjwa wa nje (OPD) 33 na tumeweza kujenga nyumba za watumishi wa afya 34," amesema Kibiti.
Kibiti ameongeza kuwa kila mwaka GGML imekuwa ikipeleka watu takribani 50 kwenda kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambapo kampuni imekuwa ikilipa takribani Dola za Kimarekani 5,000.
"Fedha zikishakusanywa zinapelekwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa ajili kusaidia watu wanaoishi na VVU lakini pia katika hii ya afya kuna watoto zaidi ya 100 ambao wamenufaika ba huduma ya afya ya upasuaji wa midomo sungura," amesema.
Kibiti ameongeza kuwa asilimia 75 ya mgodi huo ipo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Geita ambapo imekuwa ikihakikisha inasimamia ardhi na mahusiano na kuufanya msitu unakuwa vizuri na panapohitajika kufanya uharibifu wanaitwa watu wa maliasili na kulipa gharama.
Amesema GGML imekuwa na mahusiano vizuri na wachimbaji wa kati ambao wanamiliki leseni zao kihalali.
"Kunakuwa na changamoto ndogo za wachombaji wadogo kuvamia lakini sisi huwa tunawaita tunazungumza nao kwa njia rafiki na wanaondoka eneo la wanalokuwa wamevamia bila kutumia silaha," amesema Kibiti.
Naye Mtaalam wa Afya na Usalama wa Geita Gold Mining Limited, Volentine William, amesema kampuni hiyo imekuwa ikizingatia suala la afya na usalama kwa wafanyakazi ili wanapoingia na kutoka wawe salama.
"Kampuni ya GGML imeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi katika Mkoa wa Geita, tunawakaribisha watu waje katika banda letu wajifunze teknolojia za kisasa za uchimbaji ambazo hazileti athari za kimazingira na kwa jamii,"amesema William.
Kwa upande wake Afisa Raslimali Watu, Andrew Mazula, aliwataka wanawake kuchangamkia nafasi za kazi zinazotangazwa katika mgodi huo na kuondokana na fikra kwamba kazi za migodini zinafanywa na wanaume tu.
"Mgodi wa Geila Gold Mine una wafanyakazi 2,330 na kati ya hao wanawake wapo 306 tu hivyo utaona ni jinsi gani wanawake walivyo wachache katika sekta ya madini kwa hiyo tunawaomba nafasi zinapitangazwa wanawake wajitokeze kuomba kazi," alisema.
Naye Afisa Uokoaji GGM, Eliamsuri Kawiche, amesema kampuni inavyo vifaa vya kisasa vya uokoaji kunapotokea janga lolote kwenye mgodi.
MWISHO.
0 Comments