Israel imezuia bidhaa zote kuingia Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema misaada inawaishia wapalestina wa ukanda wa Gaza baada ya Isarel kuzuia misaada yote kuingizwa katika eneo hilo na kurejea kufanya mashambulizi makali dhidi ya Hamas.
Bwana Guterres amesema Gaza imegeuzwa uwanja wa mauaji na raia wanajikuta katika mkondo usiokuwa na kikomo wa vifo.
Matamshi yake yanakuja baada ya wakuu wa mashirika sita ya Umoja wa Mataifa kutoa wito wa dharura kwa viongozi wa dunia kuchukua hatua za haraka kuhakikisha chakula na mahitaji mengine yanawafikia Wapalestina.
Hata hivyo, Wizara ya mambo ya nje ya Israel inasisitiza kuna chakula cha kutosha Gaza na kumshutumu Guterres kwa kuichafulia jina Israel.
Israel iliizuia Gaza tarehe 2 Machi, baada ya hatua ya kwanza ya usitishaji mapigano kumalizika.
Hamas ilikataa kupanua sehemu hiyo ya mapatano, ikiishutumu Israel kwa kukataa ahadi zake.
Israel kisha ilifanya upya mashambulizi yake ya angani na mashambulizi ya ardhini tarehe 18 Machi na haya yameua Wapalestina 1,449, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza.
Jeshi la Israel linasisitiza kuwa halilengi raia.
Katika hotuba yake kwa waandishi wa habari, Guterres alisema Israel, kama mamlaka inayotawala, ina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuhakikisha kuwa chakula na vifaa vya matibabu vinawafikia wakazi.
"Njia ya sasa ni mwisho - haiwezi kuvumiliwa kabisa mbele ya sheria na historia ya kimataifa," alisema Guteress.
Vita hivyo vya Gaza vilichochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kurudishwa Gaza kama mateka.
Zaidi ya Wapalestina 50,810 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu wakati huo, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.
0 Comments