Na Moses Ng'wat, Songwe.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe kimewataka makada wake wanaojipitisha kwa wapiga kura kabla ya wakati rasmi wa kampeni kuacha mara moja, kikisisitiza kuwa chama kina “macho na masikio makubwa mno” yanayofuatilia kila hatua.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 28, 2025, na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo katika Mkoa wa Songwe, Mwalimu Yusuph Rajab, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi ya vikao vya maadili vilivyoketi kujadili migogoro ya ndani ya chama, ikiwemo mgogoro kati ya Mbunge wa Momba, Kondesta Sichalwe, na Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) Wilaya ya Momba.
“Tupo kwenye mwaka wa uchaguzi. Chama chetu kina utaratibu wa kuomba nafasi, kuwapitia waombaji, na uteuzi, lakini sasa tunaona kuna watu wanajipitisha kwenye majimbo na kata...CCM ina macho na masikio makubwa mno – tunawaona, tunawasikia, na tunawafuatilia,” alisema Rajab.
Rajab alisema wanachama hao wanapaswa kuelewa kuwa chama hakitavumilia uvunjaji wa taratibu, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kufanya kampeni za mapema.
“Sio kwamba hatujui, tunafuatilia kila hatua na watambue kuwa majina yanayorudi ni matatu tu safari hii tuko makini kuliko wakati mwingine wowote,” aliongeza.
Aidha, Rajab alisisitiza kuwa CCM itaendelea kushikilia misingi yake ya nidhamu, utii na maadili, na kwamba chama hakitakuwa na masihara kwa wale wanaokiuka taratibu zake.
“Tunasema wazi, tusije kulaumiana. Utaratibu wa ndani ya chama chetu uko wazi. Tufuate sheria, mila na utamaduni wa CCM,” alihitimisha.
Mwisho.
0 Comments